Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi ametangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo, baada ya mchezo wa hatua ya fainali ya michuano ya mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) dhidi ya Chile, uliochezwa mapema hii leo.

Messi ametangaza maamuzi ya kuachana na Argnetina, dakika chache baada ya kukosa penati katika mchezo huo na kuiwezesha Chile kutangaza ubingwa wa Copa America kwa mara ya pili mfululizo.

“Kwangu mimi timu ya taifa ndio basi, nimejitahidi kadri niwezavyo, inaumiza kushindwa kuwa sehemu ya mabingwa wa michuano hii,” alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29.

Katika mchezo huo Argentina walilazimishwa sare ya bila kufungana katika muda wa dakika 120, na kupelekea penati kupigwa ambapo katika hatua hiyo Chile waliibuka na ushindi wa peneti 4-2.

Hii inakua ni mara ya tatu mfululizo kwa timu ya taifa ya Argentina kutinga katika hatua ya fainali tangu mwaka 2014, ambapo walicheza dhidi ya Ujerumani kwenye michuano ya kombe la dunia na kukubali kupoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.

Mwaka 2015 katika fainali za Copa America walifungwa na Chile kwa changamoto ya penati 4-1, na mwaka huu wamefanya hivyo kwa kuambulia kichapo cha penati 4-2.

Henrikh Mkhitaryan Akaribia Kutua Old Trafford
50 Cent akamatwa kwa kutoa 'tusi' kwenye mji wa wastaarabu