Na Allawi Kaboyo Kyerwa- Kagera

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, amewaomba wananchi wilayani Kyerwa mkoani Kagera  kumchagua ili aboreshe uchumi wao kupitia kilimo, biashara na uvuvi.

Prof. Lipumba ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni leo septemba 24, 2020 katika mji mdogo wa Nkwenda wilayani humo.

Amesema wilaya ya Kyerwa ni wilaya ambayo imebahatika kuwa na ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kustawisha mazao ya aina yote ingawa wananchi wa wilaya hiyo bado ni masikini.

Mwanasiasa huyo mkongwe ameongeza kuwa ubora wa ardhi na uwepo wa mipaka ya Tanzania, Uganda na Rwanda inapaswa kuwa fursa kwa watanzania waishio maeneo hayo katika kuchochoe maendeleo yao kwa kutafutiwa masoko ya mazao badala ya kuyauza kwa njia ya magendo.

“Ndugu zangu wa Kyerwa niwaombe mnichague mimi na chama changu ili niweze kutengeneza serikali yenye kuinua uchumi wa kila mtanzania kama ilivyo ahadi ya chama chetu ya kuwa haki sawa kwa wote, wilaya hii wananchi wake hamtakiwi kuwa masikini wala kulia kwa changamoto ya kukosa maji safi na salama pamoja na miundombinu ya barabara wakati mnazo rasilimali nyingi za kuwainua,” amesema Prof. Lipumba.

“Octoba 28, mwaka huu ni siku muhimu ya kuamua mustakabali mzima wa maisha yenu, naombeni kura na nitakapokuwa Rais nitaanza na barabara hii ya kwenda mpakani kwa kiwango cha kimataifa ili iwe kichocheo cha uchumi wa watu wa Kagera lakini na kuweza kuongeza uchumi wa nchi kwa ujumla na uzuri mimi ni mwananuchumi wa kimataifa,” ameongeza.

Prof. Lipumba ameanza ziara yake ya kuomba kura kwa kufanya mikutano mkoani Kagera ambapo jana alikuwa wilayani Muleba na leo anafanya mikutano ya kampeini katika wilaya za Kyerwa na Karagwe.

Auawa kuzuia kusambaa virusi vya corona- Korea Kaskazini
Mwanafunzi amshambulia mwalimu