Sakata la mvutano wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) limechukua sura mpya baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kuingia ndani ya ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam kama Mwenyekiti.

Taarifa kutoka katika ofisi hizo zimeeleza kuwa Profesa Lipumba aliwasili na kulakiwa na umati wa wafuasi wake kabla ya polisi kumfungulia mlango kwa nguvu.

Imeelezwa kuwa Profesa Lipumba amefikia uamuzi huo baada ya kupokea barua ya maamuzi ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi ikieleza kumtambua kama Mwenyekiti halali wa chama hicho.

Wanachama wa CUF waliompokea Profesa Lipumba

Wanachama wa CUF waliompokea Profesa Lipumba

Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amekiri kupokea barua ya msajili wa vyama vya siasa na kueleza kuwa bado wanaisoma na kutafakari kilchoandikwa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa vyovyote vile Msajili wa vyama vya siasa hana mamlaka kisheria ya kuingilia maamuzi ya vikao vya chama cha siasa.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti mwaka jana kabla ya uchaguzi mkuu akipinga chama hicho kumuunga mkono Edward Lowassa kama mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na Ukawa. Lakini mwaka huu aliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa chama hicho kutengua uamuzi huo na kurejea kwenye nafasi yake.

Baraza Kuu la CUF lilimsimamisha uanachama Lipumba na viongozi wengine 10 kwa kosa la kuingilia kikao cha Halmashauri Kuu na kusababisha kikao hicho kuvunjika.

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akisisitiza kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa CUF aliwasilisha barua ya malalamiko yake kwa Msajili wa vyama vya siasa ambaye ametoa majibu yanayoaminika kuwa ya kumtambua.

Taifa Stars Kujipima Na Ethiopia
Video: Mpango wa DC Mgandilwa kuhusu usafi Kigamboni