Kada wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amekosoa utendaji wa Rais John Magufuli katika sekta ya Uchumi akieleza kuwa mapungufu yanayoonekana yasipofanyiwa kazi yatayumbisha zaidi uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF,  Buguruni jijini Dar es Salaam, Lipumba alieleza kuwa Rais Magufuli ndio chanzo cha kuadimika kwa sukari nchini kutokana na uamuzi wake wa kusitisha ghafla utoaji vibali vya kuingiza sukari nchini.

“Agizo alilolitoa Rais Magufuli Februari 28, 2016 wakati akiwashukuru waandishi wa habari, wasanii na makundi yaliyoshiriki kwenye kampeni zake za uchaguzi 2015 ndilo lililosababisha haya,” alisema Lipumba.

“Kauli ya serikali ya kuzuia utolewaji wa vibali vya uingizwa wa sukari kutoka nje ndiyo iliyosababisha upungufu wa sukari, asiuaminishe umma kuwa sababu ni wafanyabiashara kuficha sukari,” aliongeza.

Aidha alisema kuwa kutokana na vitisho vya kutumbua majipu, baadhi ya watendaji wakiwemo mawaziri na washauri wa Rais Magufuli wanaonekana kumuogopa na kwamba huenda wakashindwa kumueleza ukweli kuhusu maoni yao kitaalam kuhusu muelekeo wa uchumi.

“Rais anahitaji aelewe uchumi wa soko shirikishi, awape nafasi wahusika, asifanye maamuzi kwenye mikutano ya siasa au hadhara,” alisema Mwanasiasa huyo mkongwe.

Alimshauri Rais Magufuli kuomba ushaurii kutoka kwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa kuhusu masuala ya kiuchumi na kujenga utawala wa serikali.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alikosoa uamuzi wa vyombo vya dola kujikita katika kusaka wafanyabiashara walioficha sukari, akieleza kuwa wameacha kufuatilia masuala ya msingi kama Tegeta Escrow.

Lipumba ambaye alijiudhuru nafasi ya Uenyekiti wa CUF mwaka jana, alielezwa kushangazwa na kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kufanya kazi ya kusaka sukari zilizofichwa na wafanyabiashara.

Video Mpya: Madee - Migulu Pande
Lady Jay Dee amuandikia barua nzito Gardner, Ampa nafasi ya Mwisho