Mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaja waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa unaokikumba chama hicho.

Akizungumza jana katika mahojiano na Clouds Fm, Profesa Lipumba alisema kuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wachache wa CUF walikaa Zanzibar na kubariki kumpokea Lowassa bila kumshirikisha yeye alipokuwa Mwenyekiti wa chama hicho.

Alisema kuwa ingawa Chadema walikuwa wanaendelea kujadili suala la Lowassa kujiunga na chama hicho, CUF walikuwa tayari wamesharidhia kumpokea mwanasiasa huyo kugombea nafasi ya urais kupitia Ukawa bila kumshirikisha.

Anasema alibaini kufanyika kwa mkutano huo baada ya Lowassa mwenyewe kumuuliza kama anafahamu mjadala huo.

“Nilikuwa nakubali Lowassa aingie Ukawa lakini sio kuwa mgombea wa Urais. Kiongozi wa Taifa anahitaji kuwa na msimamo, hawezi kuwa anaongozwa na upepo tu kwamba ukitaka urais unaangalia chama gani kinaweza kukusimamisha kama mgombea,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza kuwa Ukawa walikuwa wamekubaliana kuwa mgombea urais atatoka miongoni mwao na sio nje.

Katika hatua nyingine, Lipumba alipinga hoja inayoelezwa kuwa ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa ulisaidia chama hicho kupata wabunge wengi, akidai kuwa idadi kubwa ya wabunge hao ilitokana na ujenzi wa msingi wa chama hicho kwa muda mrefu.

Profesa Lipumba alidai kuwa kitu kingine kilichomfanya amkatae Lowassa ni kwa sababu alikuwa mmoja wa wabunge wa Bunge la Mabadiliko ya Katiba lakini hakuwa anaunga mkono hoja za Ukawa za kuitetea rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.

Aidha, Profesa Lipumba ambaye ameendelea kudai kuwa yeye ndiye Mwenyekiti halali wa CUF licha ya kuwa alijiuzuru mwaka jana kupinga ujio wa Lowassa, ameapa kuwa hatakubali kuona Lowassa anakinunua chama hicho kwa bei chee akiwa nje ama ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, hoja hizo za Profesa Lipumba zilipingwa vikali na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ambaye alidai kuwa mwanasiasa huyo ni kigeugeu na kwamba anadanganya umma.

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freema Mbowe alisema kuwa haamini kama maneno anayoyasikia yametoka kwenye kinywa cha Profesa Lipumba.

Kabla ya kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa CUF mwaka jana, Lipumba laikuwa miongoni mwa Wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa walioshiriki mkutano na vyombo vya habari kumtambulisha rasmi Lowassa ndani ya umoja huo, kuwania Urais kwa tiketi ya Chadema huku akisaidia kujibu na kupangua maswali ya waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo.

lowassa-na-ukawa-lipumba

 

Mahakama Kuu yazuia NHC kupiga mnada Mali za Mbowe
Video: Mfumuko wa bei za bidhaa wapungua kwa asilimia 4.9 mwezi Agosti