Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemshambulia Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad baada ya Baraza Kuu la chama hicho kutangaza kumsimamisha uanachama yeye pamoja na viongozi wengine 10.

Profesa Lipumba amedai kuwa Maalim Seif amekuwa akikiendesha chama hicho kwa mfumo wa kiimla (udikteta) na kwamba hiyo ndiyo sababu inayomfanya kutoelewana na Katibu Mkuu (Bara), Magdalena Sakaya ambaye pia amesimamishwa uanachama.

“Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) anamdharau na hampi heshima yake Naibu Katibu Mkuu Bara,” alisema Profesa Lipumba.

“Mara nyingi huamua mambo yake bila kushirikisha viongozi wengine, halafu sasa anataka kufukuza wanachama, huwezi kuwa na chama halafu ufukuze wanachama, wanachama wanatafutwa duniani kote, halafu wewe unawafukuza, hizo ni dalili za uongozi wa kiimla, kuongoza chama unapaswa kujali demokrasia na siyo kuwa dikteta ndani ya chama,” mwanasiasa huyo mkongwe anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisisitiza kuwa yeye bado ndiye Mwenyekiti halali wa CUF na kwamba Mkutano wa Baraza Kuu uliofikia maamuzi ya kumvua uanachama haukuwa halali kikatiba.

Alikiri kuwa alijiuzulu nafasi hiyo lakini aliandika barua tena ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake. Alisema awali Maalim Seif alimwambia asubiri aombe ushauri wa kisheria, lakini baadaye aliona unatangazwa uchaguzi wa Mwenyekiti mpya bila suala lake kujadiliwa.

Kuhusu vurugu zilizoibuka katika Mkutano Mkuu Maalum wa CUF baada ya yeye na wafuasi wake kuingia ukumbini, alisema alifika pale kwa lengo la kujieleza lakini hakupewa nafasi.

Profesa Lipumba pia alidai kuwa hamtambui Julius Mtatiro ambaye Baraza Kuu lilimteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF kwa muda, akidai anachofahamu yeye bado ni mjumbe wa Kamati Kuu tu.

“Mtatiro hawezi kuwa mwenyekiti, mimi ndiye mwenyekiti wa chama, Mtatiro alishindwa hata kuongoza mkutano mkuu, ukavurugika, hawezi, simtambui,” alisema.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu akieleza kutoridhishwa na uamuzi wa chama chake kukubali kuungana na vyama vingine vya siasa vilivyounda Ukawa, kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais.

GK aukacha muziki wa Rap
Lowassa avunja rekodi Polisi, Kamanda Sirro anena