Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF), anayetambuliwa na Ofisi ya Msajii wa Vyama vya siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba amewataka wananchi wa kata ya Isagehe Wilayani Kahama, kutomchagua kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), katika ngazi ya udiwani kwa kuwa wanaweza ‘wakamuuza’ kama walivyofanya kwa Dkt. Wilbroad Slaa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
Amesema hayo  katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani wa chama cha wananchi CUF , Saidi Juma uliofanyika ndani ya kata ya Isagehe Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Lipumba amesema Chadema ilimpitisha Dkt. Slaa kuwa mgombea urais, lakini Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe alimuuza kisha kumpatia nafasi hiyo aliyekuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, kwa tamaa ya fedha.
“Msichague viongozi wapiga dili kwani mkimchagua diwani anayetoka Chadema naye anaweza kuuzwa kama Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe alivyomuuza Dkt. Slaa Uchaguzi Mkuu uliopita mkaanza kuhangaika kutafuta maendeleo, chagueni kiongozi kutoka CUF atakayesimamia rasilimali za wanaisagehe,” amesema Lipumba.
Kwa upande wake, Mgombea wa kiti hicho cha Udiwani Saidi Juma, amesema kuwa atahakikisha anatekeleza yale yote aliyoahidi wakati wa kampeni ikiwa ni pamoja na kumshirikisha Profesa Lipumba katika kumshauri namna ya kuongoza kata na kutafuta wafadhili ili kata ipate maendeleo ya haraka.

 

Trump aanza na mfuko wa bima wa Obamacare,asema anapunguza mzigo serikalini
Jammeh akubali kuachia madaraka