Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba amekituhumu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuendesha hujuma za kukivuruga chama chake.

Akizungumza jana katika kikao cha ndani kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Profesa Lipumba alisema kuwa anazitambua njama za Chadema na kwamba wanachokifanya ni kupoteza muda tu kwani chama hicho kiko imara.

“Chadema wanajitahidi kutuvuruga kwa kutumia waasi wa chama hiki, lakini naomba niwaambie hawawezi, CUF ni ngangari hata serikali inajua na  wanachokifanya ni kupoteza muda bure, alisema Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine, Lipumba aliikejeli oparesheni ‘Ukuta’ ya Chadema akidai kuwa ilikuwa dhaifu huku akiifananisha na ukuta wa biskuti.

“Unajenga Ukuta wa biskuti, ukiumwagia juisi unamong’onyoka, Ukuta gani huo, huu muziki wa CUF ni ngangari hawauwezi,” Msomi huyo anakaririwa.

Profesa Lipumba alieleza kuwa kwa kipindi chote ambacho kesi ya Uenyekiti wa chama hicho itakuwa ikiendelea mahakamani, ataendelea kushirikiana na wanachama wa chama hicho kukijenga ili kufikia malengo ya kushika dola mwaka 2020.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji alisisitiza kuwa chama chake kitasimama imara kuhakikisha CUF ambayo ni mshirika wake kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),  haiyumbishwi na mgogoro uliozuka baada ya Profesa Lipumba kurejea na kudai nafasi yake ya Uenyekiti.

Makamba achukua hatua kuokoa Ziwa Rukwa, apiga 'stop' kilimo kwenye kingo
Audio: Mbowe akumbuka UKUTA, Asema Serikali inaendeshwa kwa hila