Hatimaye Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa kukutana uso kwa macho ofisini na Profesa Ibrahim Lipumba baada ya Baraza Kuu la chama hicho kutangaza kumfuta uanachama mwanasiasa huyo (Lipumba) anayeendelea kudai kuwa ndiye Mwenyekiti halali.

Wanasiasa hao walioijenga CUF kabla ya kugeuka kuwa mahasimu katika siku za hivi karibuni, wanatarajia kukutana kesho katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizoko Buguruni jijini Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali wa chama hicho wanatarajia kuzulu ofisi hizo huku Profesa Lipumba akiahidi kuwapokea.

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa  Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Mbarara Maharagande amesema kuwa viongozi wanaotarajia kufika ofisini hapo kesho mbali na Maalim Seif ni Wajumbe wa Baraza Kuu, wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho pamoja na wabunge wake.

“Wanachama wa CUF wa Mkoa wa Dare Salaam kwa kushirikiana na wabunge wote wa CUF wameandaa mapokezi haya makubwa yatakayofanyika kesho Ijumaa, Septemba 30 kuanzia saa mbili asubuhi,” alisema Maharagande.

Alisema wajumbe wa Baraza Kuu watakakuwa wanatoka kwenye kikao kilichofanyika Zanzibar, ambacho kilifikia maazimio ya kumfukuza uanachama Profesa Lipumba.

Hata hivyo, Profesa Lipumba ambaye amekuwa akidai kuwa kikao hicho hakikuwa halali na hatambui maamuzi hayo zaidi ya kuukubali ushauri wa Msajili wa vyama vya siasa ulionesha kumtambua yeye kama Mwenyekiti halali wa CUF, alisema kesho atampokea Maalim Seif na kumkabidhi mpango kazi wa kujenga chama.

“Naamini siku atakayokuja tuatampokea na kumpeleka ofisini kwake kwa ajli ya kuchapa kazi, lakini pia nitampa mwongozo mwongozo wa namna ya kukijenga chama ikiwa ni pamoja na kumwabia kuwa fedha zisitutenanishe,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF mwaka jana lakini mwaka huu aliandika barua ya kutengua uamuzi wake na kudai kuwa bado ni Mwenyekiti halali wa chama hicho kikatiba licha ya kusimamishwa na baadae kufukuzwa uanachama.

Alirejea ofisini mwezi huu baada ya wafuasi wake kuvunja mlango na kuwashambulia walinzi wa ofisi za chama hicho, kitendo ambacho kimetumiwa pia na Baraza Kuu kama sababu ya kumvua uanachama.

Mbowe awageuzia kibano kampuni iliyomtimua kwenye jengo la NHC
Wakimataifa Wanyanyua Mikono, Kukaa Meza Moja Na Simba