Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alizua sintofahamu Bungeni wakati akiwasilisha hoja za kambi rasmi ya upinzani kuhusu utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imetimiza miezi sita.

Lissu ambaye ni waziri kivuli wa Sheria na Katiba alikosoa mwenendo wa serikali hususani utaratibu wa kutumbua majipu watumishi wa umma.

Alisema kuwa kukosekana kwa tangazo rasmi la serikali la ukasmishaji wa madaraka kwa mawaziri kumepelekea mawaziri na viongozi wengine wa ngazi za juu kuwasimamisha kazi na kuwahamisha watumishi bila kufuata sheria na taratibu wakitumia vibaya kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

Lissu aliwashauri watumishi waliosimamishwa bila kufuata utaratibu wafungue mashauri mahakamani kutafuta haki zao.

Aliwakosoa washauri wa kisheria wa Rais ikiwa ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kwa kushindwa kumshauri Rais kuandaa tangazo la kurasmisha madaraka kwa mawaziri na kulitoa kwenye gazeti la Serikali kwa mujibu wa sheria. Alisema washauri hao ni ‘majipu’ yanayofaa kutumbuliwa.

Aidha, Lissu alimvaa Rais John Magufuli akidai uwa amekuwa akifanya maamuzi bila kufuata sheria za nchi na kwamba ana viashiria vya utawala wa kiimla [udikteta].

“Serikali inaendeshwa kama mali binafsi ya Rais bila kuheshimu sheria, na ana viashiria vyote vya utawala wa kiimla na anaelekea kutokuwa na washauri katika masuala ya katiba na sheria,” alisema Lissu.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipinga vikali kauli za Lissu na kueleza kuwa Rais anafuata sheria kuwasimamisha watumishi wote kwani anafanya hivyo ili wapishe uchunguzi. Masaju alisema kuwa kama kuna mtumishi hakuridhika na kusimamishwa kwake anapaswa kwenda mahakamani.

Lissu alizua sintofahamu tena wakati akieleza kuwa Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa ikitumia mabavu kusimika viongozi ambao wanawataka wao huku akigusia mvutano wa Meya wa jiji la Tanga na mvutano uliokuwa umetokea katika chaguzi za Meya jijini Dar es Salaam.

Alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar Serikali ilitumia mabavu kuhakikisha wapinzani hawashindi huku akidai kuwa Tanganyika imekuwa ikiwasimika viongozi ambao ni vibaraka wao.

Kauli hiyo ilimuinua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju ambaye alimtahadharisha Lissu kutotumia lugha isiyo na heshima kwa Rais wa Zanzibar.

“Unamtaja Rais wa nchi [Zanzibar] kuwa ni kibaraka! Huoni ni kumdhalilisha na kumvunjia heshima yake. Tutumie lugha fasaha kulinda sifa ya mihimili mingine,” alisema Masaju.

Azam FC Wasuburi Ofa Ya Deportivo Tenerife
Jamuhuri Kiwelu Julio Awabwatukia Viongozi Wa Simba