Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ameeleza kuwa amebaini kuwepo njama ya kutaka kuwavua ubunge yeye na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Lissu alieleza kuwa barua waliyoipokea ikionesha kutoka kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inaonesha dalili za kutaka kuwavua ubunge wao kwa kutumia mianya ya sheria.

“Wanataka kutushtaki kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ili tukipatikana na hatia tukose sifa za kuwa wabunge,” alisema Lissu.

Kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma ni sehemu ya makosa ambayo yanaweza kupelekea Mbunge kukosa sifa ya kuendelea kuwa mbunge.

Aidha, Lissu ambaye aliikosoa vikali barua hiyo akidai haifanani kama imeandikwa na mtu aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, akidai kutoeleza makosa waliyofanya na kwamba haioneshi tarehe  alisema wataijibu barua hiyo kwa kuikataa.

“Barua haina maelezo yoyote ya kile kinachodaiwa kuwa kosa, haitaji tarehe, siku, muda au mahali kosa hilo lilipotendeka,” alisema Lissu kuhusu barua hiyo aliyoeleza kuwa imeonesha kuandikwa na Jaji Mstaafu, Salome Kaganda ambaye ni Kamishna wa Maadili na Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, Jaji Kaganda alifanya mahojiano juzi na mwandishi wa habari wa gazeti moja la kila siku na alikana kufahamu lolote kuhusu barua hiyo.

“Mimi sifahamu lolote kuhusu suala hilo na sina taarifa,” alisema Jaji Mstaafu Kaganda.

Mbowe na Lissu wanatuhumiwa kutoa makatamko ya kichochezi kwa nyakati tofauti wakitangaza operesheni Ukuta ambayo wamepanga kuifanya Septemba 1 kwa kufanya mikutano na maandamano nchi nzima.

Olympic 2016 Yawaunganisha Korea Kusini Na Kaskazini
Ni Real Madrid Tena, Waigaragaza Sevilla CF