Serikali imejikuta ikikwaa kisiki tena Mahakamani katika kesi ya uchochezi dhidi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kutupilia mbali maombi ya kutaka Wakili Peter Kibatala asimtetee mbunge huyo.

Lissu alifikishwa Mahakamani hapo Agosti 5 mwaka huu akikabiliwa na kesi ya uchochezi, lakini upande wa Serikali uliiomba mahakama kuamuru Kibatala ambaye ndiye kiongozi wa Jopo la Mawakili wanaomtetea Lissu kujitoa katika jopo hilo na badala yake kuwa shahidi wao (Serikali).

Akisoma uamuzi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema kuwa Mahakama hiyo haikubaliani na ombi la upande wa Serikali na badala yake inakubaliana na hoja ya Wakili Kibatala kuwa hakuna kifungu chochote kinachomzuia kumtetea Lissu kwa sababu tu alishuhudia tukio hilo.

Hakimu Mkeha aliongeza kuwa endapo Serikali itataka kumtumia Kibatala kama shahidi wao italazimika kumuomba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 19.

Awali, Serikali ilikwaa kisiki mahakamani hapo ilipotaka kuzuia Lissu asipewe dhamana. Baada ya kusikiliza pande zote hadi majira ya saa tatu usiku, Mahakama iliridhia kumpa Lissu dhamana na kutupilia mbali hoja za mawakili wa Serikali.

Mfanyabiashara ajiua kwa kujilipua na Petroli
CCM wataka Maalim Seif azuiwe kuhudhuria matukio ya kitaifa