Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kuwa tayari ameshalipwa mishahara na stahiki zake za kibunge kwa kipindi cha tangu mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.

Lissu ambaye awali alilalamika kuwa mshahara wake umesimamishwa pamoja na stahiki nyingine kutokana na maagizo ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu mwenendo wake akiwa nje ya nchi na mambo aliyokuwa akiyasema dhidi ya nchi, amesema kuwa amesitisha mpango wake wa kwenda Mahakamani baada ya kulipwa fedha hizo.

Spika Ndugai alisema kuwa Lissu hajawasilisha ripoti ya maendeleo ya matibabu yake kinyume cha taratibu na kwamba anaonekana akiwa anazurura katika nchi mbalimbali akiisema vibaya Serikali. Hivyo, alimshauri arejee nyumbani badala ya kufanya jambo hilo ambalo alisema ni kuichafua nchi.

“Nilisema nitaenda Mahakamani kama hawatalipa mshahara na posho zangu za kibunge, kama wameshalipa suala la kwenda Mahakamani halipo tena,” amesema Lissu alipofanya mahojiano na Mwananchi.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye ni mwanasheria alisema kuwa bado ana mpango wa kwenda Mahakamani kudai gharama za matibabu yake lakini atafanya hivyo baada ya kurejea nchini kwani yeye ndiye mshtaki na shahidi muhimu kwenye suala hilo.

Lissu anapatiwa matibabu nchini Ubelgiji kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya kupigwa risasi nje ya nyumba yake maeneo ya Area D jijini Dodoma, Septemba, 2017.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameeleza kuwa anaendelea vizuri na matibabu na kwamba ana mpango wa kurejea nchini kabla mwaka huu haujaisha.

 

 

Lissu: Nitarejea, sitakubali kuishi uhamishoni
Trump akaliwa kooni kuhusu ripoti ya Urusi, awaachia vumbi tu