Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi ameendelea kubanana na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anafanya ziara na mahojiano nchini humo.

Masilingi ambaye awali alishiriki kwenye mahojiano ya Lissu kwenye kipindi cha ‘Straight Talk Africa’ kinachotumia lugha ya kiingereza, jana alishiriki tena kwenye kipindi cha Kiswahili cha kituo hicho cha runinga cha Voice of America/Sauti ya Amerika akitoa majibu ya papo kwa papo ya tuhuma na hoja za Lissu dhidi ya Serikali na Bunge.

Balozi huyo aliendelea kumsihi Lissu kusitisha ziara yake na badala yake yeye na dereva wake warudi nchini Tanzania ili washirikiane na vyombo vya usalama katika kusaidia uchunguzi wa tukio lake la kupigwa risasi, Septemba 7, 2017.

Hata hivyo, Lissu aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa sheria za nchi zinaruhusu jeshi la polisi kumhoji mtuhumiwa au shahidi akiwa nje ya nchi kwa kushirikiana na serikali za nchi  husika.

Aidha, Balozi Masilingi alionesha kuchukizwa na lugha aliyotumia Lissu dhidi ya sababu zilizotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye mahojiano hayo, na kumsihi kuheshimu vyombo vya dola.

“Huyu ni mwanasheria mwenzangu, ni Mtanzania mwenzangu, umesikia lugha anayotumia ‘ni ujinga mtupu’, kwa vyombo vya dola ambavyo vinachunguza kupata hatma ya shambulio la jaribio la mauaji ya binadamu hata kama sio Tundu Lissu,” alisema Masilingi.

“Kutotambua kazi nzuri ya Serikali na unazunguka dunia nzima unatukana Rais wako, unatukana nchi yako, unatukana vyombo vya dola, unatukana Watanzania kwamba ‘hakuna haki pale..,” aliongeza.

Masilingi alipinga hoja ya Lissu kuwa Jeshi la polisi linapaswa kuendelea na uchunguzi hata kama hayupo, akimtaka kutotumia kisingizio cha nini kingefanyika kuhusu uchunguzi endapo angepoteza maisha.

“Anasema kama angekufa…! hakufa sasa,” alisisitiza.

Lissu ambaye alipinga maelezo ya Balozi Masilingi akidai kuwa anachofanya ni kukosoa Serikali. Alisema kuwa bado hajapona na kwamba anategemea kufanyiwa upasuaji mwingine.

“Siwezi kuzungumza kwa asilimia lakini naweza nikasema naendelea vizuri. Sijapona kwa sababu tarehe 20 ya mwezi huu ninaenda kufanyiwa oparesheni nyingine, oparesheni ya 23. Kwahiyo sijapona lakini naendelea vizuri,” alisema Lissu.

Wiki hii, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam iliwataka wadhamini wa Lissu kuwasilisha ripoti ya maendeleo ya afya ya Lissu anayeshtakiwa mahakamani hapo kwani hakuna taarifa zozote za kidaktari kwenye rekodi za Mahakama.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alionesha kukubaliana na hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Geita, Joseph ‘Msukuma’ Kasheku ya kusitisha mshahara wa Lissu kwani hakuna ripoti ya maendeleo yake kiafya wakati anaonekana akiwa anafanya ziara ughaibuni.

Hatua hiyo ilipingwa vikali na Chadema kupitia taarifa yao iliyotolewa jana, wakidai kuwa huko ni kuonesha chuki dhidi ya mbunge huyo.

Video: Bunge kusimamisha mshahara wa Lissu, Serikali yafunguka nyongeza mishahara
Video: Drake, Meek Mill waandika rekodi wakifunikana ‘Going Bad’