Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesaini mkataba maalum na kampuni ya kimataifa ya kisheria ya Amsterdam and Partners LLP akiwapa jukumu la kusimamia haki zake za kikatiba na za kimataifa.

Kampuni hiyo imetoa taarifa yake jana, Oktoba 2, 2019 ikieleza kuwa imefurahi kufanya kazi na Lissu ambaye ni mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

“Tunajivunia kufanya kazi na Tundu Lissu katika kuongeza uelewa kwenye hali yake na kampeni dhidi ya uvunjifu wa sheria na haki za kisiasa,” imeeleza kampuni hiyo.

Lissu ambaye yuko nchini Ubelgiji tangu Januari 6, 2018 alipoenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na kujeruhiwa kwa risasi, alitangaza kuahirisha kurejea nchini Septemba 7 mwaka huu kama alivyoahidi ili akutane kwa mara nyingine na madaktari wake.

Mwanasiasa huyo alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa maeneo ya nyumbani kwake, Area D jijini Dodoma.

Alipatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kisha akapelekwa jijini Nairobi kwa matibabu zaidi, kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji alikoendelea kupatiwa matibabu hadi leo.

Kampuni ya Amsterdam and Partners LLP yenye makazi yake jijini London nchini Uingereza, kazi yake kubwa ni kuwashauri wateja hususan kwenye changamoto kubwa za kisheria.

Kifo cha Khashoggi kuadhimishwa nje ya ubalozi alimopotelea
Mkuu wa mkoa awacharaza bakora wanafunzi 14 kwa kumiliki simu shuleni