Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anatarajia kuanza ziara yake katika nchi mbili za Ulaya pamoja na Marekani kuanzia kesho, ikiwa ni siku chache tangu Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka asitishe ziara hizo na kurejea nyumbani.

Kengele hiyo ya wito uliotolewa na Ndugai iliambatana na tahadhari kuwa mbunge huyo anayepatiwa matibabu nchini Ubelgiji tangu Januari 26 mwaka jana kutokana na tukio la kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka juzi, hana ruhusa ya Ofisi ya Bunge ya kuwa nchini humo na kumkumbusha kuwa Spika “ana nguvu zake katika hilo.”

Jana, Afisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene alitoa taarifa inayoeleza kuwa Lissu ambaye anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji, atafanya ziara katika nchi za Ujerumani, Ubelgiji pamoja na Marekani kuanzia kesho.

Katika taarifa hiyo, Makene alieleza kuwa Lissu atazuru Ujerumani kwa siku mbili ambapo atakutana na wabunge wa bunge la nchi hiyo. Baada ya kurejea Ubelgiji atazuru Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya jijini Brussels ambapo atakutana na Wabunge wa Umoja huo pamoja na baadhi ya wanadiplomasia.

Ziara ya mwanasiasa huyo ambaye ni mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani itaishia jijini Washington nchini Marekani ambako atakutana na Shirika la Msaada la Watu wa Marekani (USAid) na Kamati za Mabunge ya Marekani zinazohusika na uhusiano wa Nje.

Akiwa Marekani, Lissua anatarajia kutumia siku 10 ambapo atakutana pia na Wamarekani waishio nchini humo katika majimbo ya Texas, Houston, Alabama na Washington.

Januari 19, Spika alisema, “Yeye ametoka kuugua, aache uzushi arudi nyumbani tunamsubiri. Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,” alisema Ndugai muda mfupi baada ya Lissu kufanya maojiano na BBC kupitia ‘Hard Talk’.

Ibara ya 71 (1)(C ) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mjadala kuhusu suala hilo, ambayo inaeleza kuwa Mbunge akikosa kuhudhuria vikao vya mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika atakoma kuwa Mbunge.

Hata hivyo, Lissu alijibu kauli ya Spika Ndugai akieleza kuwa asingeweza kuomba ruhusa wakati alisafirishwa kwenda Nairobi akiwa hajitambui baada ya kushambuliwa kwa risasi na kwamba Spika alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kikao cha dharura kilichotoa uamuzi wa kumsafirisha.

Sakata hilo na mjadala uliokuwa unaendelea hasa mitandaoni lilimuibua Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume aliyetafsiri ibara hiyo kwa kulinganisha na kinachoendelea na aliiambia Idhaa ya Kiswahili ya DW, “kama Spika atatumia haki hatamvua ubunge Mheshimiwa Lissu lakini kama atatumia madaraka basi ataweza kumvua ubunge.”

Juventus yazungumzia mpango wa kumsajili Pogba
Serikali kujenga Chuo Cha VETA mkoani Kagera