Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amewakumbuka watu waliookoa maisha yake baada ya kupigwa risasi Septemba 17, 2017 jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika viwanja vya Zakhem jijini Dar es Salaam uliofanyika mwishoni mwa juma, Lissu aliwashukuru watu watatu waliomkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Alimtaja binti wa Naibu Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Juma Akukweti aitwaye Khadija, dereva wake Adamu Mohamed Bakari na Msaidizi wake wa nyumbani aliyemtaja kwa jina la Amina.

“Hawa ndio watu waliookoa maisha yangu, walionikimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma muda mfupi baada ya kushambuliwa kwa risasi. Huenda bila hawa watu nisingekuwa hapa leo,” amesema Lissu.

Lissu aliwashukuru pia Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya kwa jinsi alivyosimamia zoezi la kumpeleka katika hospitali ya Nairobi kwa matibabu zaidi.

Mwanasiasa huyo aliwashukuru pia madaktari wa hospitali hiyo ya jijini Dodoma; na kuishukuru dunia kwa ujumla kwa jinsi ilivyompa huduma katika nchi zote alizopatiwa matibabu kabla ya kurejea nchini Julai 27, 2020.

Lissu anawania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipeperusha bendera ya chama chake ambacho tofauti na uchaguzi wa mwaka 2015 hakitakuwa kimeungana na vyama vingine vya siasa kushindana na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi.

Katika hatua nyingine, Chadema waliamuru wafanyakazi wa TBC kuondoka katika viwanja hivyo ndani ya dakika 15, kwa madai kuwa matangazo ya mkutano wao yamekuwa yakirushwa kwa kukatwa.

Uongozi wa TBC umelaani kitendo hicho ukieleza kuwa tamko la viongozi hao lilihatarisha usalama wa watendaji wake pamoja na vifaa.

TBC wamefafanua kuwa wanarusha matangazo ya mikutano ya vyama vyote kama Sheria ya Uchaguzi inavyoelekeza na hawakipendelei chama chochote. Wamefafanua kuwa hata wakati Chadema wanatoa tamko hilo mkutano wao ulikuwa unaendelea kurushwa mubashara kupitia TBC.

Hivyo, wamekilalamikia chama hicho kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kueleza kuwa itasitisha kurusha matangazo ya mikutano yao hadi watakapohakikishiwa usalama.

Mwanamke mwenye miaka 42 akamatwa kwa kumbaka mvulana wa shule ya msingi
Faida zitokanazo na Choroko

Comments

comments