Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alizua mjadala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya Hakimu kumtaka Mwanasheria wa Serikali kueleza kwanini hajakamatwa.

Mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa kwa Lissu kutokana na kushindwa kuhudhuria bila kutoa taarifa katika kesi ya uchochezi inayomkabili.

“Kwanini hakumkamata, si mlikuwa na wajibu wa kumkamata… mnamuogopa?” Alihoji Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Kutokana na hali hiyo, wakili wa Serikali, Patrick Mwita alimuomba radhi Hakimu kwa kutomkamata Lissu huku akieleza kuwa mbunge huyo ambaye pia ni mwanasheria mbombezi alifanya dharau kutotoa taarifa kwa maandishi kuwa hajafika mahakamani kwakuwa anasimamia kesi ya uchaguzi wa jimbo la Bunda Mjini katika Mahakama Kuu.

Naye Hakimu Simba alieleza kuwa Lissu ni mwanasheria maarufu na msomi anayejua taratibu zote za kimahakama hivyo anatakiwa kujua kuwa mahakama haimuogopi wala haitamuonea. Aliahirisha kesi hiyo hadi itakaposikilizwa tena Novemba 28 mwaka huu.

Lissu na watu wengine watatu wanakabiliwa na kesi ya uchochezi kutokana na chapisho kwenye gazeti la Mawio kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar.

Abracadabra Awaburuza Tena Sweden
Lowassa, Sumaye waizawadia Chadema Mkakati wa CCM