Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, amesema Serikali ndiyo yenye wajibu wa kumtafuta na kumpata raia wake, Ben Saanane,  ambaye amepotea kwa miezi ipatayo miwili sasa.

Aidha, Lissu amekanusha uvumi unaoenezwa kwamba huenda chama chake kinahusika katika kupotea kwa  mtu huyo, ambapo amesema katika kukwepa kusema kitu kisichojulikana, wameitaka  Serikali kutoa tamko iwapo inafahamu Mtanzania huyo aliko au haifahamu.

“Mpaka sasa Serikali haijasema lolote kuhusiana na jambo hilo.  Tunafahamu Ben amepotea lakini wakati mwingine tunanyamaza kwa sababu tunachokifahamu sisi ni sawa na mnachokifahamu nyie ila nawahakikishia kwamba hatuhusiki kwa vyovyote na kupotea kwake,” amesema Lissu.

Aidha, Lissu amesisitiza kuwa msimamo wa chama chake wa kuzitaka Mamlaka zote husika na Usalama wa raia ziseme hali halisi inayozingira sintofahamu hiyo ya mahali alipo Saanane ikiwa yuko ndani au nchi za nje, au hata kama amefariki na kuzikwa kwa kutotambuliwa.

Hata hivyo, Lissu amesema kuwa kutoonekana kwake Arusha kusaidia juhudi za kumpatia dhamana Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema kuna wanasheria wengi wa chama hicho wanaoweza kufanya kazi hiyo lakini akasema suala hilo linaonekana gumu kwa vile linaendeshwa kisiasa.

Mpinga: Tutakamata magari yote yenye taa zenye mwanga mkali
Kesi ya uhujumu uchumi yakwama