Baada ya muda mrefu wa klabu ya Liverpool kusubiri kwa takribani miaka 30, usiku wa kuamkia leo walifanikiwa kutwaa ubingwa wa kwanza kabisa wa Ligi Kuu nchini England (EPL).

Ndoto ya miaka 5 ambayo walikuwa wameiota kwa kumchukua kocha Jurgen Klopp akitokea Borrusia Dortmund imefanikiwa kujibu bila shida baada ya msimu wa mwaka jana mbio za kufikia ukingoni jioni kwa Manchester City kuwaacha kwa alama chache.

Majogoo wa Jiji la Merseyside wamefanikiwa kutwaa taji la EPL bila kukanyaga uwanja, kwani baada ya mchezo wao dhidi ya Crystal Palace walioshinda goli 4-0 (Juzi Jumatano), walikuwa wanahitaji alama mbili pekee kuwa mabingwa, lakini balaa lililomkuta aliyekua bingwa mtetezi Manchester City mbele ya Chelsea likawa faraja kwao.

Manchester City wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya EPL, walikubali kichapo cha mabao mawili kwa moja kutoka kwa Chelsea, na rasmi wameutema ubingwa.

Ni taji la 19 la Liverpool na ubingwa wa kwanza kwao, tangu walipotwaa taji hilo mwaka 1989-90.

Licha ya katazo la kusalia nyumbani lililotolewa na Meya wa Jiji kutokana na uwepo wa janga la virusi vya Corona lakini maelfu ya mashabiki walijikusanya nje ya dimba la Anfield na kushangilia ubingwa wao wa kwanza kabisa kwa miaka 30.

Wachezaji wa Liverpool ambao walikuwa wanaangalia mechi ya City dhidi ya Chelsea walionekana wakishangilia pamoja wakiwa hotelini, mlinzi Virgil van dijk, kipa Alisson, kiungo mshambuliaji Alex Oxlade-Chamberlain ni miongoni mwa wachezaji wa Liverpool walionekana wakishangilia.

Klopp, akiwa amevalia tisheti yenye ujumbe wa kusifia safari yao ya kuchuchumilia taji alisema “Sina cha kusema, siamini kilichotokea”.

“Imekuwa zaidi ya nilivyofikiria, kuwa bingwa katika klabu hii ni zaidi ya furaha isiyokuwa na kifani”.

“Sikuwa hapa kwa hiyo miaka 30, nimekuwa hapa kwa takribani miaka 5 lakini haikuwa kazi rahisi kupata mafanikio haya tuliyoyapata sasa, hasa baada ya mapumziko ya miezi mitatu hakuna aliyejua kama ligi ingerudi tena”. Aliongeza Jurgen Klopp ambaye msimu uliopita 2018/2019 aliipa taji la kwanza la Ulaya Liverpool baada ya miaka mingi pia.

Kocha wa zamani wa Liverpool Kenny Dalglish alikuwa kocha wa mwisho kutwaa ubingwa wa 16, 17 na 18 lakini tangia hapo miaka 30 imepita bila taji, wamepita makocha wengi, wamepita wachezaji wengi lakini bado hawakufanikiwa kupata mafanikio makubwa mpaka mwaka 2015 ambapo walimpa kandarasi ya miaka mitano kocha Jurgen Klopp ambapo ameifanikisha kutwaa taji la 19.

Burundi: Nkurunziza kuzikwa leo
Simba, Young Africans zatakiwa kufuata nyayo za KMC FC