Majogoo wa jiji Liverpool wamekataa ofa ya Euro milioni 100 iliyotumwa na FC Barcelona kwa ajili ya uhamisho wa kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Philippe Coutinho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la Telegraph la nchini England, FC Barcelona walituma ofa hiyo kwa kuwaomba Liverpool wakubali kiasi cha Euro milioni 85 na kisha watamalizia Euro milioni 15, kwa makubaliano ya kiwango cha mchezaji huyo pindi atakapojiunga na Barca.

Bila kupoteza muda Liverpool wameikataa ofa hiyo kwa kuendelea kusisitiza mchezaji huyo hauzwi katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

FC Barcelona wanahaha kumsaka Coutinho kwa lengo la kuziba nafasi ya mshambuliaji Neymar, ambaye juma lililopita alikamilisha mpango wa kuondoka Camp Nou na kujiunga na matajiri wa jijini Paris nchini Ufaransa PSG.

Coutinho mwenye umri wa miaka 25, alisajiliwa na Liverpool mwaka 2013 kwa ada ya Pauni milioni 8.5 akitokea Inter Milan ya Italia, tayari ameshaweka wazi mpango wa kutaka kujiunga na FC Barcelona lakini akaweka msimamo wa kutowasilisha ombi la kuondoka Liverpool.

Kauli hiyo ya Coutinho inaaminisha maamuzi ya mwisho ya uongozi wa Liverpool ndio yataamua hatma yake ya kuondoka klabuni hapo ama kubaki klabuni hapo, kwa mujibu wa mkataba aliousaini mwezi Januari mwaka huu.

Mbrazil huyo alisaini mkataba wa miaka mitano wa kuendelea kuitumikia Liverpool, na atakua huru kuondoka Anfield mwaka 2022.

Garry Monk: Ben Gibson Hauzwi
Majaliwa apiga marufuku ununuzi wa Tumbaku kwa dola