Majogoo wa Jiji ‘Liverpool’ wametwaa Ubingwa wa FA, kwa kuizaba Chelsea katika mchezo wa Fainali uliounguruma leo Jumamosi (Mei 14).

Miamba hiyo ya England ilipapatuana Uwanja wa Wembley jijini London na kushindwa kufungana ndani ya dakika 120, hivyo iliilazimu kufika kwenye hatua ya Penati.

Hili ni taji la nane la FA kwa miamba hiyo ya Anfield.

Liverpool ilifanikiwa kuibuka wababe wa mchezo huo na kutwaa Taji la FA kwa kupata Mikwaju ya Penati 6-5.

Nahodha Cesar Azpilicueta na Mason Mount walikosa kwa upande wa Chelsea huku Sadio Mane ndiye pekee aliyekosa kwa upande wa Liverpool.

Hii ni mara ya pili kwa timu hizo kufika hatua ya Penati, kwani zilipokutana katika mchezo wa Fainali Kombe la Ligi ‘Carabao Cup’ zilishindwa kufungana na sheria hiyo ilitumika huku Liverpool ikiibuka mwamba.

Ni bahati kwa klabu hiyo ya Anfield msimu huu kucheza Fainali mbili ndani ya England, huku Fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ikitarajiwa kushuhudiwa ikicheza dhidi ya Real Madrid mjini Paris-Ufaransa baadae mwezi huu.

Liverpool ilitinga Fainali ya michuano hiyo kwa kuifunga Villareal ya Hispania, huku Real Madrid wakiiondoa Manchester City ya England.

Je? Liverpool wataendelea kukusanya taji la tatu kwa msimu huu baada ya kutwaa Carabao Cup na FA Cup katika ardhi ya nchini kwao England? Ama Real Madrid wataongeza taji la pili kwa msimu huu baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania?

Tusubiri na kuona nani ataibuka Mwamba wa Ulaya msimu huu katika Jiji la Paris-Ufaransa

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 15, 2022
Majaliwa awataka Gas Entec kuzingatia makubaliano ya mkataba