Meneja wa majogoo wa jiji, Liverpool, Jurgen Klopp ameitaka bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo kufanikisha usajili wa mshambuliaji kutoka nchini Mexico, Javier Hernandez ‘Chicharito’ wakati wa majira ya kiangazi .

Taarifa iliyotolewa na ITA Sport Press, imeeleza kuwa, Klopp ameridhishwa na uwezo wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 na atapendezwa sana endapo atamuona katika kikosi chake msimu wa 2016/17.

Klopp, amemuingiza Chicharito katika mipango yake, kufuatia washambualiaji wa wake wa sasa, Christian Benteke, Daniel Sturridge na Danny Ings kukabiliwa na changamoto ya majeraha sambamba na kuporomoka viwango kwa kiasi cha kuhangaika kupata mabao.

Hata hivyo huenda Liverpool wakapata upinzani mkali kutoka kwa klabu ya Arsenal ya England pamoja na Bayern Munich ya Ujerumani  ambazo zinatajwa kumuwinda Chicharito.

Klabu ya Manchester United iliafiki kumuachia Chicharito mwanzoni mwa msimu uliopita, kutokana na meneja wao Louis Van Gaal kutokumkubali katika mipango yake.

Chicharito alijiunga na Bayer Leverkusen mwezi agosti mwaka jana, baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo akiwa na Real Madrid ya nchini Hispania na mpaka sasa ameshapachika mabao 22 katika michezo 26 aliyocheza akiwa nchini Ujerumani.

Raphael Varane Kuwa Wa Kwanza Kutua Man Utd 2016-17
Neymar Aanza Kuzigombanisha Man Utd, Man City