Meneja wa Manchester United Louis van Gaal amesema hakuna muujiza wa kuimarisha hali ya klabu hiyo na lazima wahusika wote watie bidii.

United wamecheza mechi nane bila kushinda hata moja, sita zikiwa ligini, na kushuka hadi nambari sita.

Aidha, wameondolewa kutoka Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

“Hakuna muujiza, siri ni kuangalia yaliyotokea na kuona ni wapi tunaweza kujiboresha, kama timu na kama watu binafsi,” amesema, klabu hiyo ikijiandaa kukabili Swansea Jumamosi.

“Nimeshindwa mara tatu na Swansea, na baadaye unadadisi ni kwa nini ulishindwa. Mambo huwa hivyo, kisha unaendelea na mzunguko mwingine wa kufanya kazi.

“Unaweka mpango wa kulaza mpinzani wako na lazima ushawishi wachezaji wako. Baadaye, lazima ufanye mazoezi hadi uridhike. Kisha ujitolee na kujaribu kutekeleza mpango huo.

United walitoka sare 0-0 na Chelsea Jumatatu, mechi ambayo walionekana kucheza vyema baada yao kulazwa 2-0 na Stoke City siku ya Boxing Day.

Kabla ya mechi hiyo dhidi ya Chelsea, kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda Van Gaal akafutwa baada ya klabu hiyo kuandikisha msururu wa matokeo mabaya.

Alipoulizwa iwapo sare hiyo ilimpunguzia shinikizo, alisema: “Sijui kwa sababu shinikizo huwa kwako na wachezaji pia.”

United waliongoza ligi muda mfupi 21 Novemba baada ya kulaza Watford, mechi yao ya mwisho kushinda, lakini sasa wamo alama tisa nyuma ya viongozi Arsenal.

Van Gaal hata hivyo amewashukuru mashabiki kwa kuendelea kumuunga mkono.

“Hii si klabu yangu ya kwanza, labda itakuwa ya mwisho, ambapo nimepitia kipindi kibaya. Nimekuwa na vipindi vibaya na klabu zote nilizopitia na ninaweza kusema mashabiki hapa Manchester United ndio bora zaidi.

Van Gaal hata hivyo anaamini mwaka 2015 umekuwa mwema kwa klabu hiyo.

 

Simba Kusaka Furaha Ya Mwaka Mpya Mjini Mtwara
Farid Mussa Kusaka Maisha Hispania