Meneja wa Man Utd, Louis Van Gaal, amewatahadharisha mashabiki wa klabu hiyo wenye sifa ya kuzomea zomea, kwa kuwaambia wajiandae kumuona tena msimu ujao.

Van Gaal amefikisha ujumbe kwa kundi hilo la mashabiki, alipokua akitoa maneno ya shukurani kwa mashabiki waliohudhuria katika mchezo wa kufunga msimu wa 2015-16, ambao ulishuhudia Man Utd wakiibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya AFC Bournemouth.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, alisema anaamini kipindi cha mpito alichopitia tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Man Utd, kimekua fundisho kwake na atahakikisha anafanya kila jitihada za kusaka matokeo mazuri msimu ujao ambao utaanza rasmi mwezi ogasti mwaka huu.

“Natambua uwepo wa mashabiki wanaonipinga kila wakati, na jambo hilo linatokana na matokeo mabaya tuliyoyapata kwa msimu huu, lakini imekua fundisho kwangu na tutakua sote msimu ujao,”

“Sisi sote ni wamoja na sioni sababu ya kunyoosheana vidole ama kila mmoja kumzomea mwingine, ninakuhakikishieni nimejifunza mengi na tayari ninajua wapi tulipojikwaa, kwa hiyo tuwe tayari kwa msimu ujao ambapo naamini tutaimarika zaidi.” Alisema Van Gaal

Van Gaal, mwenye umri wa miaka 64, bado ana jukumu la kukiongoza kikosi cha Man Utd katika mchezo wa hatua ya fainali wa kombe la FA ambao utaunguruma mwishoni mwa juma hili katika uwanja wa Wembley.

Katika mchezo huo Man Utd watapambana na Crystal Palace.

Petr Cech Atwaa Gloves Za Dhahabu
Serikali kufungia matumizi ya mitandao ya kijamii ofisini