Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameweka wazi msimamo wake kuwa atamuunga mkono Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga ambaye anaungwa mkono na muungano wa NASA.

Lowassa ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema, aliweka wazi msimamo wake kumuunga mkono mgombea huyo wa chama tawala nchini Kenya jana kijijini kwake Ngarash wilayani Monduli, alipokuwa akizungumza na wageni wakiongozwa na wabunge 13 wa Kenya, viongozi wa kabila la kimasai (maleigwanan) na vikundi mbalimbali vya kijasiriamali wa nchi hiyo.

“Mimi na familia yangu tunamtumikia Mungu lakini vilevile kwa dhati kabisa sisi wana Monduli tunamuunga mkono Uhuru Kenyatta kwenye mbio za Urais nchini Kenya,” Lowassa anakaririwa na Tanzania Daima.

“Naomba nitamke wazi na dunia yote ijue kuwa sisi tunampenda Uhuru Kenyatta naye anatupenda, kwa hiyo tunamuunga mkono kwa kuwa tunaamini ana uwezo wa kuwaunganisha Wakenya na Watanzania,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa muda muafaka ukifika yeye na familia yake wataenda nchini Kenya kumuunga mkono Kenyatta kwenye kampeni za uchaguzi wa nchi hiyo.

Mwaka 2013, Rais John Magufuli, akiwa waziri wa ujenzi, alienda nchini Kenya na kupanda jukwaani kumpigia debe rafiki yake Raila Odinga katika mbio za uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, msimamo wa Lowassa huenda ukakinzana na msimamo wa chama chake cha Chadema ambacho mwaka 2013 kilionesha kumuunga mkono Odinga kama mgombea wa chama cha upinzani, katika uchaguzi uliomalizika kwa kumpa ushindi Uhuru Kenyatta kuwa rais halali wa Kenya.

Ikumbukwe kuwa Lowassa ni kiongozi mkuu wa Wamasai (Leigwanan) Afrika Mashariki.

Nabil Maaloul Arejea Kuipa Makali 'Eagles of Carthage'
Waamuzi Wa Soka Waigomea MZFA