Wakati harakati za kisiasa nchini zikiwa zimetulizwa kwa muda na Jeshi la Polisi, taarifa mbalimbali zinazodaiwa kutoka kwa vyanzo vinavyofichwa majina zinatumika kuendeleza propaganda hizo kimyakimya ambapo leo gazeti moja limedai kupata mpango wa Edward Lowassa kutaka kuihama Chadema.

Lowassa aliihama CCM mwaka jana na kujiunga na Chadema iliyompa nafasi ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa kihistoria ulioonesha ushindani mkubwa kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Ikiwa ni siku moja baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii waraka uliodaiwa kuandikwa na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) akidai kumkataa Edward Lowassa, waraka ambao hata hivyo ulikanushwa na Chadema, gazeti jipya la ‘Mwana Habari’ limedai kuwa Lowassa ameandaa mkakati mpya wa kuihama Chadema.

Gazeti hilo limeeleza kuwa vyanzo vya kuaminika vimesema kuwa Lowassa anataka kukirithi chama cha UDP ambacho hivi sasa kiko chini ya uenyekiti wa John Cheyo. Limeeleza kuwa mkakati huo umeanza kwa kumtanguliza rafiki yake wa karibu, Goodluck Ole Medeye ambaye tayari amekabithiwa ukatibu mkuu wa chama hicho.

Medeye ambaye mwaka jana aliihama CCM na kujiunga na Chadema, alitangaza kuhamia chama cha UDP mwaka huu akipinga utaratibu unaotumiwa na wabunge wa vyama vya upinzani kumpinga Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

“Habari zilizopatikana kutoka ndani ya chama hicho zinasema kuwa hatua ya mwanasiasa huyo kuhamia huko haikuja kama bahati mbaya, bali kilichofanyika ni kutangulizwa na Lowassa kabla yeye mwenyewe hajafanya hivyo pia,” limeandika gazeit la Mwana Habari.

Limedai kuwa chanzo kimeeleza kuwa baadae Cheyo anaweza kustaafu nafasi yake kumpisha Lowassa ambaye hivi sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, akongoze chama hicho ambacho katika uchaguzi mkuu uliopita hakikuambulia hata mbunge mmoja.

“Cheyo amechoka kisiasa na kifedha, hivyo alichokuwa anatafuta ni kupokelewa nafasi hiyo na mtu mwingine. Lakini alikuwa hajapatikana kutoka ndani ya chama chake, fursa ambaye inaonekana kuwa nzuri kwa Lowassa,” gazeti hilo linakinukuu chanzo chake.

Hata hivyo, taarifa hizo ambazo ni vigumu kuthitisha ukweli wake kutokana na kuonesha kuwa za usiri na njama zimekuja wakati ambapo Lowassa amekuwa akisisitiza kuwa amejipanga kusaidiana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kukijenga chama hicho hadi katika ngazi za matawi.

Serikali yaizika rasmi ‘Shisha’
JPM atuma salamu za rambirambi Mabasi yaliouwa 29, madereva wadaiwa kufanya mzaha