Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameeleza kile anachoamini kuwa ndio tiba halisi ya matatizo ya wizi katika sekta ya madini nchini. Amesema hayo siku chache baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya pili ya mchanga wenye madini, uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi na kampuni ya Acacia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alisema kuwa ili matatizo ya unyonyaji kwenye sekta hiyo yakabiliwe kikamilifu, Tanzania inapaswa kuandika katiba mpya.

Alisema kuwa mapungufu katika mikataba na sheria ya madini yamekuwa yakilalamikiwa na wapinzani kwa miaka mingi ndani ya Bunge lakini maoni yao hayakukubalika.

“Wapinzani wameshasema sana, wakasema mikataba hii iletwe tuitazame upya kwenye Bunge, lakini walikataliwa,” alisema akiwataja baadhi ya makada wa vyama vya upinzani kama Tundu Lissu, John Mnyika na Zitto Kabwe waliowahi kuwasilisha ombi hilo.

“Walikataliwa kwa sababu siri yake, jambo hili haliko kwenye katiba. Ndio maana mimi nasema tiba yangu moja kubwa ni kuhakikisha tunapata katiba mpya. Katiba ambayo itazitangatia maslahi ya wananchi katika kugawanya rasilimali zake,” aliongeza.

Aidha, Lowassa alimpongeza Rais John Magufuli kwa hatua alizochukua dhidi ya makampuni ya madini akieleza kuwa hata yeye aliahidi kuwa angefanya hivyo endapo angeshinda katika uchaguzi uliopita.

“Nampongeza mheshimiwa Rais John Magufuli kwa hatua alizochukua, hasa pale anapowashirikisha wananchi,” alisema na kuongeza kuwa huo ulikuwa mpango wa Ukawa tangu awali.

Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo mkongwe alitahadharisha kuwa jambo hilo linapochukuliwa hatua lisijenge chuki kwa watu na kwamba liangaliwe vyema ili lisije kuliingiza Taifa kwenye madeni kwakuwa Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa.

JPM amewafungua macho viongozi wengi wa Afrika na dunia - Dkt. Bana
?Live: Jeshi la Polisi Dar es salaam lapokea magari ya doria