Wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea kushika kasi huku kila mgombea akimwaga ahadi kila anapofika, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anaeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa ameeleza atakapotoa fedha za kutimiza ahadi nono alizozitoa.

Lowassa aliwaeleza wakazi wa Singida kuwa hatategemea misaada kutoka nje ya nchi ili kutimiza ahadi hizo bali atatumia rasilimali zilizopo nchini kwa kuwa zikisimamiwa vizuri zinaweza kukamilisha ahadi hizo kwa uhakika.

Alisema ahadi zote zilizoanishwa katika ilani ya uchaguzi ya Chadema inayoungwa mkono na Ukawa, zitakamilika pia bila kutegemea misaada ya wafadhili.

Mgombea huyo aliwaahidi wananchi kuwa endapo watamchagua atahakikisha kuwa serikali yake inatoa elimu bure kuanzia kidato cha kwanza hadi chuo kikuu, atakamilisha ujenzi wa reli ya kati kwa kuweka treni za mwendo kasi, kuligeuza jiji la Mbeya kuwa kama Singapole, kumaliza tatizo la maji jijini Dar es Salaam pamoja na kuweka treni za umeme katika jiji hilo.

Wananchi wa mkoa wa Singida walijitokeza kwa wingi kumpokea Edward Lowassa katika maeneo mbalimbali aliyofika kunadi ilani ya chama chake. Lowassa ambaye aliongozana na viongozi wengine wa vyama vinavyounda Ukawa alifanya mikutano katika wilaya ya Manyoni, Ikungi na Singida Mjini.

Lowassa aliwaomba wananchi hao kumpigia kura kwa kuwa anahitaji kura nyingi ili ashinde katika uchaguzi huo.

“Naombeni sana mnipigie kura, nimekuja kuomba kura zenu ili nilete mabadiliko… nahitaji kura milioni 10 na ushee hivi ili nishinde,”alisema Lowassa baada ya kuwahoji wananchi hao kama watampigia kura au la. Umati huo ulinyoosha mikono na kuitikia kwa sauti ya juu ‘Umepata’.

 

 

Wafikishwa Mahakama Ya Kisutu Kwa Makosa Ya Mtandao
Zitto Kabwe Awapigania Slaa Na Lipumba, Akosoa Ahadi Ya Magufuli