Waziri Mkuu wa zamani, Edward lowassa amekana tuhuma zilizoelekezwa kwake na mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 31 aliyedai kuwa ni mtoto wake na kwamba amemtelekeza.

Mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa waliofika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakidai kutelekezwa na wazazi wao au kutelekezwa na wazazi wenza.

Lowassa amesema kuwa hamtambui mwanamke huyo na kwamba kama angekuwa mwanaye kweli angekuwa amemchukua.

Akiongea kwa njia ya simu na gazeti la Nipashe, Lowassa amesema kuwa kinachofanyika ni siasa za kuchafuana na kwamba kwake kupima vina saba (DNA) kwa lengo la kutambua kama mwanamke huyo ni mwanaye ni upuuzi na kupoteza muda.

“Kupima DNA ni upuuzi. Yaani nipoteze muda wangu kwenda kufanya upuuzi huo, siko tayari,” alisema Lowassa.

“Wewe unamwamini huyo msichana? Angekuwa mwanangu kweli ningekuwa nimeshamchukua muda mrefu, kwanza wala simjui, naona siasa zimeingia hapo,” Lowassa anakaririwa.

“Anasema ameshindwa kuniona wakati ana umri wa miaka 31, wewe unaamini kweli ameshindwa kuniona? Mbona wewe umenitafuta na umenipata na unaongea na mimi kwenye simu? Hizo ni siasa zinazolenga kuchafuana,” alioongeza Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Awali, mtoto wa Lowassa, Fred Lowassa alijibu madai ya mwanamke huyo na kueleza kuwa hawamtambui na kwamba kama angekuwa ni ndugu yao angeenda kueleza kwenye ukoo wao huko Longido kwani kwao watoto ni baraka.

Akieleza mbele ya waandishi wa habari, msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma Lowassa, alidai kuwa alielezwa na mama yake kuwa baba yake ni Lowassa.

Alisema alishafuatilia hadi Ikulu kuomba kuonana na kiongozi huyo tangu akiwa shuleni lakini hakufanikiwa. Fatuma anadai aliwasilisha barua Ikulu wakati Lowassa akiwa Waziri Mkuu lakini pia hatua hiyo haikuzaa matunda.

Rais Magufuli akumbushia uimara wa Kikwete
Harry Kane apewa bao dhidi ya Stoke City

Comments

comments