Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa leo amewasili tena katika makao makuu ya jeshi la polisi jijini Dar es Salaam kama alivyoamriwa.

Lowassa ambaye alifika katika jengo hilo na kuingia katika Ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCIA), alitumia nusu saa ndani ya ofisi hizo na kutakiwa kurejea tena Alhamisi ijayo.

Mwanasheria wa mwanasiasa huyo, Peter Kibatala alisema kuwa baada ya kufika katika ofisi hizo walipewa maelekezo ya kurejea tena Alhamisi bila kupewa sababu ya maelekezo hayo.

“Lowassa kama mnavyoona amefika katika ofisi za DCI na maelekezo ni kwamba arudi tena Alhamisi tarehe 20 [Julai] saa tatu asubuhi. Kwahiyo, tutarudi na tutapata maelekezo zaidi,” Kibatala aliwaambia waandishi wa habari.

Lowassa amehudhuria kwa mara nyingine katika ofisi hizo za DCIA kwa ajili ya mahojiano kufuatia kauli yake aliyoitoa wakati wa kushiriki futari iliyoandaliwa na madiwani wa Chadema jiijini Dar es Salaam akimuomba Rais Magufuli kuwatoa gerezani mashekhe wa Jumuiya ya Uamsho kwa madai kwamba hawafikishwi mahakamani tangu walipokamatwa miaka minne iliyopita.

Kwa mujibu wa Lowassa, katika mahojiano yake ya kwanza na DCI alielezwa kuwa kauli hiyo ni ya kichochezi lakini alisisitiza kuwa anasimamia alichokisema kwani anaamini alikuwa sahihi.

Tofauti na ilivyokuwa awali, leo Lowassa alifika katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi akiwa na msafara wa magari machache, huku ulinzi wa Jeshi la Polisi katika eneo hilo ukionekana kuwa wa kawaida kwa kulinganisha na ilivyokuwa awali.

Everton yaifunga Gor Mahia, wavimbiana kama Ulaya
Said Mrisho: Nimeachana na mke wangu ila sijatelekeza familia