Zikiwa zimebaki siku 7 kabla watanzania hawajafanya maamuzi ya nani awe rais, mbunge au diwani, imethibitika kuwa wagombea wawili wa urais wenye nguvu zaidi kaidi, Edward Lowassa (Chadema) na Dkt. John Magufuli (CCM) hawatakaa meza moja kupimana nguvu kwa hoja.

Hayo yamebainishwa na Taasisi ya Twaweza ambayo imeandaa mdahalo wa wagombea urais kwa ushirikano na CEO Round Tables na Tamwa. Taasisi hiyo imeeleza kuwa vyama vinne pekee ndivyo vilivyothibitisha kushiriki katika mdahalo huo uliopangwa kufanyika Jumapili, Oktoba 18 na kurushwa moja kwa moja na vituo vya runinga nchini.

Vyama hivyo vilivyothibitisha ushiriki wa wagombea wao wa nafasi za urais ni pamoja na CCM, ACT-Wazalendo, Chaumma na ADC. Hivyo, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa hatakuwa mmoja kati ya wagombea watakaofanya mdahalo huo, hali inayodhihirisha kupungua nguvu kwa mdahalo huo.

Akitoa sababu za kutoshiriki kwa Lowassa, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu ameeleza kuwa mgombea wao anakabiriwa na ratiba ngumu ya kampeni.

“Huwezi kumuondoa mgombea kwenye kampeni aende kwenye mdahalo, akatumie siku mbili kujiandaa na kusafiri bila kuwafikia wananchi vijijini ambao wanamsubiri kwa hamu, kwa ufupi, sisi tunawatakia kila la kheri,” alisema Mwalimu.

Naye Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alieleza kuwa taasisi hiyo ilitoa fursa kwa wagombea kuulizwa na kujibu maswali ya wapiga kura wao lakini hawawabembelezi wagombea kushiriki.

Awali, Chama Cha Mapinduzi kilieleza kuwa kisingeweza kushiriki mdahalo huo kama mgombea wa Chadema, Edward Lowassa asingeshiriki wakidai kuwa mdahalo huo bila wagombea urais wote wenye nguvu hauna maana. Msimamo ambao wameuondoa na kuamua kushiriki hata bila mgombea huyo.

Magufuli: Namhurumia Dkt. Shein
Diamond Kushindana Na Mrembo Wa Dunia Toka India, Priyanka Chopra