Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye leo ametambulishwa rasmi kuwa mwanachama wa Chadema akitokea CCM, ameweka wazi kilichosababisha sakata la Richmond na jinsi alivyohusishwa na kuchukua uamuzi wa kujiuzuli Uwaziri Mkuu mwaka 2008.

Akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari waliohudhuria zoezi la kumtambulisha rasmi kuwa mwanachama wa Chadema na mshirika wa Ukawa, Lowassa ameeleza kuwa yeye ndiye mtu wa kwanza kukataa mkataba wa kampuni za kufua umeme baada ya kuzitilia shaka.

Lowassa alieleza kuwa baada ya kugundua kuwa kuna tetesi za ujanja kupitia mkataba huo ambao ulibainika kuhusisha makampuni hewa ya kufua umeme na ndipo alipoamua kuitisha kikao na Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na makatibu wakuu na kwamba baada ya kujadili aliamua mkataba huo kuvunjwa.

Alisema wakati anafanya maamuzi hayo ndani ya kikao hicho, mjumbe mmoja aliomba ruhusu ya kutoka nje ya kikao kwa muda wa saa moja akienda kuongea na simu.

Alisema baadaye mjumbe huyo alirudi ndani na kumwambia kuwa ‘mamlaka ya juu zaidi’ imeamua kuwa mkataba huo usainiwe na kwamba hayo na maagizo ya kiutawala (directives).

Aidha, Lowassa alieleza jinsi ambavyo hakuridhishwa na mchakato wa kumpata mgombea wa CCM uliopelekea jina lake kukatwa na Kamati ya Usalama na Maadili. Alisema CCM aliyoishuhudia mjini Dodoma wakati wa mchakato ule, sio CCM iliyomlea na kumfikisha hapo katika ulimwengu wa siasa.

Lowassa na mkewe walikabidhiwa rasmi kadi ya Chadema kuashiria ujio wake rasmi katika chama hicho.

Hivi ndivyo alivyoeleza Lowassa kuhusu Richmond:

“Nilijibu juzi, mtu ambaye ana ushahidi dhidi yangu kuhusu Richmond peleka mahakamani. Kama huna shut and keep quiet. Nilichukua jukumu la serikali, nikajiuzulu kwa niaba ya serikali. Hivi ni dhambi hiyo? Mimi nilidhani ningepewa medali. Kwa sababu jamani… mnakumbuka, kulikuwa na shida ya umeme nchini, mvua zilikuwa hazijanyesha tukaambiwa tutapata break up completely. Kwa hiyo tukaangaika kuleta mikataba hiyto ya kuwasha umeme. Tukahangaika tukaleta.

“Lakini in the process ikagundulika kupitia media kwamba yule mtu aliyekuwa apewe mkataba hakuwa makini, hakuwa na hela na na wakawa na mashaka na kampuni zake. Nilipopata habari hizo nikamuandikia mwanasheria mkuu wa serikali, kwamba ziko habari mitaani kuwa huyo mtu hana uwezo, nikampa nakala rais. Lakini baada ya siku tano nikaita mkutano, Katibu Mkuu kiongozi, makatibu wakuu wote waliokuwa wanahusika.

“Kusema ukweli aliyekuwa anahusika na mkataba ni Government Negoting Team. Ikiongozwa na Grey Mgonja. Waziri mkuu huendi ku- negotiate mkataba, wala hauulizwi, wanamaliza huko wanakuletea taarifa kuwa wamemaliza.

“Kwa hiyo nikaita hicho kikao nikawaambia ‘nimepata habari hizi..mbona hamchukui hatua?’ Kwa wakati ule nilikuwa nimetoka kuwa waziri wa maji, walikuwa wamekuja watu wa City kutudanganya tukavunja mkataba ule tukaenda vizuri.

“Nikawambia nina uzoefu wa kuvunja mikataba, mkataba huu tuuvunje. Akatoka nje akaomba muda wa saa moja, akawasiliana na mamlaka za juu. Akarudi akasema imeagizwa mkataba usivunjwe. What else could I have done? Lakini niliyapenda majibu ya Profesa [Lipumba] jana, tangu nilipoondoka madarakani miaka minane iliyopita mambo hayo yamepungua au yameongezeka. Kuna aliyewajibika kisiasa? Wadogo tu…! I take pride that I saved my nation, I took political responsibility na sina chochote nilichokula cha mtu yeyote…tena wakati tunasaini mkataba na tume inaundwa ya bunge ilikuwa haijalipwa hata senti moja. Kwa hiyo mikono yangu ni misafi sina chochote, na mtu mwenye ushahidi acha kupigapiga kelele, peleka mahakamani ushahidi wako.”

Watoto Wa Abedi Pele Wakamilisha Ndoto Zao
Drogba Atimkia Marekani