Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametoa shukurani zake kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuzuia mikutano ya nje na kuruhusu mikutano ya ndani kwa vyama vya kisiasa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mafunzo ya siku mbili kwa madiwani, wabunge na viongozi wa Chadema yanayoendeshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Konard Adenauer Shiftung (Kas) ya Ujerumani, Lowassa alisema kuwa baada ya kufanya mikutano ya ndani hususan katika mikoa ya Kusini, amebaini kuwa ni mizuri zaidi kuliko ya nje.

“Hali ni nzuri zaidi baada ya kufanya mazungumo na wanachama wa Chadema katika miko hiyo. Tunashukuru…Rais John Magufuli aliona hakuna haja ya vikao vya nje,” alisema.

“Tunashukuru kwa sababu ametupatia vikao vya ndani, ni vizuri na vitamu zaidi ya vikao vya nje kwa sababu unaonana na wanachama ana kwa ana kwa muda mrefu zaidi kwa mapenzi na mahaba,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Lowassa ambaye tangu alipokuwa CCM alikuwa bingwa wa mikakati ya ‘chini kwa chini’ bila kutumia mihadhara, alisema kuwa amebaini wanachama wa chama hicho bado wako imara na kwamba watakiletea ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Mwanasiasa huyo mkongwe alisema kuwa anaona dalili zote za ushindi katika uchaguzi huo lakini akatahadharisha kuwa utawezekana tu endapo wanachama wataendelea kudumisha umoja wao.

Rais Magufuli alipiga marufuku siasa za majukwaani hadi mwaka 2020 na kuruhusu mikutano ya ndani pekee, marufuku ambayo awali ilipingwa vikali na vyama vya upinzani. Hali hiyo ilipelekea Chadema kutangaza Oparesheni Ukuta ikiazimia kufanya maandamano nchi nzima Septemba Mosi mwaka huu, azimio ambalo hata hivyo liliahirishwa.

Video: Kinana, Nape kung'oka CCM, Joto la Magufuli latua...
Utafiti Mpya: Pombe ni hatari kwa Moyo wako, fahamu kiasi usichopaswa kuvuka