Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameendelea kuhimiza amani nchini huku akionesha matumaini yake kuwa siku moja ataupita mlango wa Ikulu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, aliyasema hayo jana katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa Chadema, tawi la Ubungo kwa lengo la kumpongeza kwa ukomavu wa kisiasa aliouonesha baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

“Siku moja tutaingia Ikulu bila kumwaga damu. Msiwe na wasiwasi kwa sababu mimi, dunia na Watanzania wanafahamu kuwa tulishinda katika uchaguzi uliopita,” alisema Lowassa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo wa zamani alitoa ombi lake kwa          Rais John Magufuli kuhusu mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar. Alimtaka Rais Magufuli kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza.

“Hali ya Zanzibar isiposhughulikiwa kwa umakini na umahiri, italeta matatizo makubwa nchini,” alisema. “Nashauri wakae chini wazungumze, kwa nini hili la sasa linashindikana wakati CUF walikubali Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa miaka mitano?”

Kadhalika, Lowassa aliishukia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akipinga kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Damian Lubuva kuwa iko huru.

Alisema kuwa tume hiyo inaendeshwa na chama tawala na kwamba katika uchaguzi uliopita ilipotosha matokeo na kwamba watendaji wake walipaswa kufukuzwa baada ya uchaguzi kukamilika.

Waliomdhalilisha Mtanzania India watiwa Mbaroni, Hofu yaongezeka
Mbunge wa Upinzani atimuliwa bungeni