Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amezungumzia kauli zilizokuwa zikielekezwa kwake na baadhi ya wanasiasa kuhusu afya yake na wengine kumtabiria kifo.

Akizungumza jana katika kikao cha ndani cha chama hicho mjini Mbinga mkoani Ruvuma, Lowassa ambaye hakutaja majina, alisema baadhi ya watu waliosema hayo dhidi yake walishatangulia mbele ya haki.

“Bila ujasiri na umoja wa dhati, hawa jamaa wataendelea kutupiku… lakini niwashukuru vilevile kwa kukubali kubeba lawama juu yangu, wapo waliosema huyu ni mgonjwa atakufa, bado mlinipigia kura nyingi ila Mungu ndiye hupanga yote,” alisema.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, baadhi ya wanasiasa waliopanda majukwaani waliwashawishi wananchi kutompigia kura Lowassa wakidai kuwa ni mgonjwa na kwamba hana siku nyingi atafariki dunia.

Wapo walioenda mbali na kudai kuwa ikulu hakuna gari la kubeba wagonjwa na bajeti ya msiba wa kiongozi huyo. Hata hivyo, hakuwahi kuwajibu jukwaani.

Lowassa yuko katika ziara ya mikoani kwa ajili ya kufanya vikao vya ndani vya chama hicho vilivyopewa jina la ‘Oparesheni amsha-amsha’. Wengine walioko katika ziara hiyo katika mikoa tofauti ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdallah Safari, Frederick Sumaye na wengine.

Tumetoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya elimu - Majaliwa
Magufuli amnyang’anya rasmi Sumaye shamba la Dar