Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amesema kuwa ushindi kwa umoja huo katika uchaguzi wa mwaka 2020 uko wazi kutokana na hali inavyoonekana hivi sasa.

Lowassa aliyasema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa Kamati Kuu ya Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) jijini Dar es Salaam. Alisema kuwa ushindi kwa Ukawa uko ‘nje nje’ kwa mwaka 2020 endapo vyama hivyo vitadumisha umoja wao.

“Ushindi wa upinzani mwaka 2020 upo nje nje ikiwa viongozi wa Chadema na wenzao wa Ukawa pamoja na wanachama wao watadumisha umoja na kujikita kuimarisha chama vijijini,” alisema Lowassa.

Aliwatahadharisha kuulinda umoja huo na kwamba kuna watu wameajiriwa serikalini kwa lengo la kuhakikisha wanavivuruga vyama vya upinzani.

Aidha, aliwapongeza Bavicha kwa kutiii agizo la Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwataka wasiende Dodoma kwa lengo la kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa makabidhiano ya Uenyekiti wa chama. Aliwataka kuendelea kuilinda katiba na kutotumia nguvu kushindana na matamko ya Rais Magufuli kama kuzuia mikutano ya kisiasa, badala yake wawaache CCM wapate shida ya kujieleza mbele ya wananchi kutokana na kuvunja matamko yao wenyewe.

“Kwa uzoefu wangu ndani ya CCM, wakimaliza kumpatia chama Rais Magufuli watampeleka Uwanja wa Jamhuri pale Dodoma ili kuhutubia, sasa hiyo itakuwa tayari ni mkutano wa siasa, sasa sisi ujumbe wetu umefika waacheni wapate shida kujieleza kwa wananchi,” alisema Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema.

Mwanasiasa huyo mkongwe na waziri mkuu wa zamani alisema kuwa maisha ya wananchi yamekuwa magumu tangu kuanza kwa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano na kwamba wananchi wamekosa matumaini waliyoyategemea, hivyo hawatakuwa na njia mbadala isipokuwa kufanya maamuzi katika uchaguzi ujao.

Ali Kiba, Barakah Da Prince wavamiwa na watu wenye bunduki Afrika Kusini
Video: Naibu Waziri Atoa Wito Huu Kwa Watanzania