Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewajibu baadhi ya watu waliomshauri kujiuzulu siasa baada ya mgombea wa Chadema aliyekuwa anampigia debe kushindwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Monduli.

Kati ya waliomshauri Lowassa kustaafu ni pamoja na aliyewahi kuwa waziri wa Kilimo na Mifugo na Mbunge wa zamani wa Bunda, Stephen Wassira.

Akizungumza na Dar24 baada ya kushuhudia uzinduzi wa Sera za Chadema wiki hii jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema kuwa wanaomtaka afanye hivyo wanaota.

“Huyo [anayetaka nistaafu siasa] anaota,” alisema Lowassa akijibu swali hilo kwa ufupi.

Aidha, akijibu kuhusu matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Monduli ambalo aliliongoza kama mbunge kwa miaka 20, alisisitiza kile alichowahi kukisema, “nilishatoa maoni yangu hata kwenye magazeti ukasome… nilisema kwa tume hii hakuna chama kingine ambacho kitashinda uchaguzi.”

Mwanasiasa huyo mkongwe pia alisema kuwa ataendelea kutoa ushauri wake kwa Chadema katika vikao vya ndani vya chama, akikataa kuzungumzia ushauri huo kwenye vyombo vya habari.

Lowassa aliweka kambi Monduli akimpigia kampeni mgombea wa Chadema, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Julius Kalanga kuhamia CCM na kugombea tena ubunge.

Kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya uchaguzi, Kalanga alishinda kwa asilimia 95 ya kura zote.

Video: Mdee anena ya viongozi Chadema kutodhuria mazishi MV Nyerere
Ole Sendeka atuma salamu za rambrambi kwa JPM