Mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameendelea kutangaza neema ya kuboresha huduma ya afya nchini akilenga zaidi wanawake na watoto.

Akihutumia wakazi wa wilaya ya Moshi, Lowassa alieleza kuwa serikali yake itahakikisha inapunguza vifo vya akina mama na watoto kwa kupeleka huduma bora zaidi za afya karibu na wananchi kwa kuzibadili hospitali za wilaya kuwa hospitali za rufaa.

“Nina usongo na hospitali za serikali. Kwanza tabu wanazopata watu hasa akina mama ni tabu sana. Nimekusudiwa nikichaguliwa kuwa rais nitafanya hospitali za wilaya kuwa referral hospital (hospitali za rufaa). Zitakuwa na madaktari mabingwa, tutawasomesha wengi wa kutosha,” alisema.

Katika hatua nyingine, Lowassa aliwatangazia neema wakazi wanaoishi mipakani ka kuahidi kuboresha ushirikiano na nchi za jirani pamoja na kuwaruhusu kuuza bidhaa zao hasa za kilimo katika nchi yoyote endapo wataona bei ya mazao nchini haiwaridhishi.

Lowassa alimjibu mpinzani wake mkubwa, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli kwa kumtaja akieleza kuwa atakachokifanya katika zoezi hilo ni kutengeneza ajira na sio kuondoa ajira kama alivyodai (Magufuli).

“Nitaondoa kabisa ushuru kwenye mazao, sitaki kusikia mkulima anasumbuliwa na habari za ushuru. Ukitaka kupeleka mazao yako Kenya nenda, ni rukhsa. Mtu aliye na Kahawa yake na haina bei Tanzania, peleka Rwanda, peleka Uganda.

“Magufuli anasema oooh mnaharibu ajira, siharibu ajira, ndio natoa ajira..! kwa kufanya hivyo, biashara za mipakani zikomae, fanyeni biashara, hapana kuogopa,” alisisitiza.

Lowassa anaendelea na kampeni zake ambapo leo anatarajiwa kufanya mikutano katika jimbo la Karatu kabla ya kuelekea Musoma ambapo atafanya mkutano mjini humo kesho (Oktoba 11).

 

NEC Yaeleza Ukweli Wa Mashine Za ‘BVR’ Zilizokamatwa Dar
Magufuli Kuibadili Bagamoyo ‘Falme Za Kisasa’