Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amesema hali ya chakula hivi sasa hapa nchini ni mbaya na kuna uwezekano wa kutokea baa la njaa.
 Ameyasema hayo mjini Bukoba akiwa kwenye ziara yake ya kuimarisha chama, amesema kuwa hali ya chakula ni mbaya na kuna uwezekano mkubwa nchi ikakumbwa na baa la njaa, Lowassa amemuomba Rais Magufuli kutozipuuza hoja zinazotolewa kuhusiana na masuala mbalimbali ya nchi.
“Eneo moja ambalo hakika rais anatakiwa kusikia hoja za watu wengine ni suala la njaa, nimeshuhudia mwenyewe pale Longido na maeneo mengine, hali ya mvua ni mbaya, hali ya chakula ni mbaya, watu wako hoi halafu wanaambiwa hakuna kuwapelekea chakula,” amesema Lowassa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema Taifa lina msiba wa njaa na amekuwa akipokea taarifa kutoka kwa wabunge wengi na ni vyema Serikali ikalifanyia kazi.
“Hili tatizo lipo na pale unapokuwa unawazuia binadamu kusema ipo siku mawe yatazungumza na ukweli utabainika kile ambacho Watanzania walikuwa wana kizungumzia kipo. Hifadhi ya chakula hapa nchini ilianzishwa ili kusaidia wakati wa majanga ya njaa, sasa leo kuna tatizo na wananchi wanasema lakini maneno yao yanakuwa yanapuuzwa, si jambo la kiungwana,” amesema Mbowe.

Mashindano ya vikundi vya mazoezi kuanza jijini Dar es salaam
Somalia yapiga marufuku ndoa za kifahari, ni baada ya kugundua jambo