Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema aliyeungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amepanga kutoa kile kilichodaiwa kuwa ni siri nzito kuhusu kilichotokea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Lowassa amepanga kutoa tamko zito kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 na utangazaji wa matokeo ikiwa ni siku chache baada ya kueleza kutokubaliana na matokeo ya urais akidai kuwa matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na NEC yalitofautiana na matokeo waliyokuwa wameyapata kwenye vituo husika.

Taarifa zilizotolewa jana kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Ubunge za Chadema katika jimbo la Arusha Mjini zinaeleza kuwa Lowassa pia leo atatoa ujumbe mzito na msimamo wa Ukawa kuhusu kinachoendelea visiwani Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta uchaguzi mkuu Oktoba 29.

Lowassa hakuweza kuhudhuria katika uzinduzi wa Kampeni jijini Arusha na kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo Godbless Lema kama ilivyoahidiwa. Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alieleza kuwa Lowassa alishindwa kuhudhuria kutokana na kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Novemba 15 ambapo atatoa tamko zito.

Waziri Mkuu huyo wa zamani sasa anatarajia kuhudhuria katika ufungaji wa kampeni za ubunge wa Arusha Mjini.

 

Dkt. Nchimbi, Ndugai, Mpambano Mkali Uspika
Madeko ya Kanye West Yampa Mawazo Kim Kardashian Kuhusu Mtoto wa Pili