Yakiwa yamebaki masaa kadhaa kabla watanzania hawajapiga kura kushiriki kwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu, mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa amepanga kuhutubia Taifa kupitia vyombo vya habari, leo majira ya saa tatu usiku.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene, Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Lowassa atazungumza na Watanzania wote, ndani na nje ya nchi, na watu wa mataifa yote, kuhusu Tanzania mpya itakayotokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo, kiutawala na utendaji wa serikali atakayoiunda baada ya Watanzania kumpatia dhamana ya kuwa Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi Mkuu wa Serikali, Oktoba 25.

“Aidha, Mhe. Lowassa atatumia muda huo kuwashukuru Watanzania wote kwa namna walivyomuunga mkono kwa upendo mkubwa yeye, mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji, chama na UKAWA kwa ujumla katika uchaguzi huu wa mabadiliko, ya kuhitimisha utawala wa nusu karne wa CCM kuliandaa taifa na uongozi mpya utakaotoa utumishi wa kuliondoa taifa hapa lilipokwama katika umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi unaowatafuna Watanzania,” alisema Makene.

Katika hatua nyingine, Jana Lowassa alijitabiria ushindi wa asilimia 80 kwa kile alichodai hali na muamko aliouona katika maeneo aliyopita wakati wa kampeni.

“Kuna watu wanasema nitapita kwa asilimia 51, lakini mimi kwa hali niliyoiona, kwa mapokezi niliyoyapata vijijini kwa vijana, wazee na akina mama… nadhani ni asilimia 80,” alisema huku akiwaomba wananchi kumhakikishia ushindi huo.

Ronaldo Aanza Kumgaragaza Messi Kabla Ya 2016
Baada Ya CCM Kutangaza Safu Ya Wafunga Kampeni, Chadema Yaanza Kutangaza Safu Kuwakabili Mikoani