Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa anatarajia kutoa alichonacho moyoni kwa Watanzania wote baada ya kushindwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25.

Waziri mkuu huyo wa zamani anatarajiwa kupanda jukwaani kuhutubia Jumamosi hii ikiwa ni mara ya kwanza tangu kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanikisha kupatikana kwa Rais wa serikali ya awamu ya tano, Dkt. John Magufuli kwa tiketi ya CCM.

Lowassa atamnadi mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema katika mkutano wa kampeni utakaofanyika Jumamosi hii jijini humo.

Kwa mujibu wa mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, Lowassa na viongozi wengine wa Ukawa watatoa tamko zito siku hiyo hivyo aliwataka watanzania kwa ujumla kutega sikio.

Katika hatua nyingine, Lema aliwataka wananchi wa jimbo la Arusha Mjini kutoendelea kuhuzunika na kutokata tamaa kutokana na matokeo ya uchaguzi wa rais bali waungane pamoja.

“Ndugu zangu msikate tamaa, nasikia kuna watu wameanza kutupa shahada zao, hapana msifanye hivyo, ndio kwanza kazi inaanza na lolote linaweza kutokea kwa uwezo wa Mungu,” alisema Lema.

Lema alieleza kuwa uamuzi wa Lowassa kutokutoa tamko la kuhamasisha kupinga matokeo ya uchaguzi kuliliepusha taifa na machafuko badala yake Ukawa waliamua kutumia vyombo vya kimataifa.

“Tunaendelea kutumia Taasisi za kimataifa kudai haki, ndio sababu mnaona Zanzibar wameshindwa kujitangazia matokeo, hii ni kazi kubwa ya Ukawa,” Lema anakaririwa.

Uchaguzi wa jimbo la Arusha uliahirishwa kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Estomih Mallah.

Uchaguzi umepangwa kurudiwa Desemba 13 mwaka huu.

 

Jese Rodriguez Amtamanisha Arsene Wenger
Afrika Yapata $1.9 Bilioni Kuzuia Wanaokimbilia Ulaya, Tanzania Yaguswa