Mjumbe mpya wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ameeleza kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichokitumikia tangu mwaka 1977, ni kejeli, mipasho, kusakamwa, kushambuliwa, kutishiwa kwa kuitwa ‘gamba’ na fisadi.

Lowassa alisema kuwa operesheni zilizoanzishwa za kuvua gamba zililenga katika kumtishia na kuzua kejeli na vijembe dhidi yake hali anayoamini ilikuwa ya kumuonea na kumfanya awe na sababu ya kukihama chama hicho na kutorejea tena.

Mwanasiasa huyo ambaye alikihama CCM siku chache baada ya jina lake kuenguliwa kati ya wagombea waliokuwa wanawania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais, na kujiunga na Chadema waliompa nafasi hiyo, alieleza kuwa pamoja na hayo bado anakiheshimu chama chake.

“Nakifahamu Chama cha Mapinduzi, nakiheshimu kwani ndicho kilichonilea, lakini, kwa hali tuliyokuwa tumefikia, inafika mahali unasema imetosha,” alisema Lowassa jana katika mahojiano maalum ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Lowassa alisema kuwa mbali na hilo, sababu nyingine iliyomfanya akihame chama hicho ni kutaka kuleta mabadiliko katika nchi. Alisema hata Mwalimu Julius Nyerere alieleza kuwa mabadiliko yasipopatikaa ndani ya CCM yatapatikana nje ya CCM hivyo alitoka nje ya chama hicho ili kuleta mabadiliko hayo.

Alisema hivi sasa anajikita zaidi katika kukiimarisha chama chake hicho kipya kuanzia katika ngazi za mashina ili kujiandaa na uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

“Sina mpango na wala siwezi kurejea CCM, mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, na jukumu lililoko mbele yangu ni kukijenga na kukiimarisha chama changu hiki kiwe imara tangu katika ngazi ya matawi,” alisema na kuongeza kuwa Chadema wamepanga kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga kura wao kwa kura nyingi walizowapa ikiwa ni sehemu ya harakati za ku kukiimarisha chama hicho.

Lowassa anaamini kuwa alishinda katika uchaguzi uliopita na kwamba kilichofanyika na uchakachuaji wa matokeo.

Alisema moja kati ya vitendo vilivyomuumiza moyo ni hatua ya kukamatwa kwa vijana wa Chadema waliokuwa wakijumlisha matokeo na kuwekwa mahabusu.

Katika hatua nyingine, Lowassa alipinga uamuzi wa kuzuia TBC kurusha matangazo yote ya bunge moja kwa moja akidai kuwa hatua hiyo ni kuminya demokrasia. Pia, alikosoa kitendo cha polisi na mbwa kuingia bungeni kuwatoa wabunge wa upinzani.

Alisema kuwa hivi sasa wabunge wa upinzani wana kazi nyingine ya kudai katiba mpya ya wananchi Bungeni na nje ya Bunge, katiba itakayoweka Tume huru ya Uchaguzi kwani iliyopo sio huru hata kidogo.

 

Mbowe anamng'ata na Kumpuliza Zitto? aeleza sababu ya kumtosa Uwaziri Kivuli
Mawaziri wa Zamani, Mramba na Yona wahukumiwa kufanya usafi Hospitalini, kifungo cha nje