Sakata la uuzwaji wa nyumba za serikali uliofanyika mwaka 2002 hadi 2004 limechukua sura mpya baada ya kuwahusisha pia mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Akichangia katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati (CCM), alisema kuwa nyumba hizo za Serikali ziliuzwa kwa watumishi wa umma wakiwemo Frederick Sumaye na Lowassa ambao hivi sasa ni wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

“Nyumba za Serikali ziliuzwa mwaka 2002, Waziri Mkuu alikuwa Sumaye na aliuziwa plot namba 68, na Lowassa aliuziwa plot namba 590,” alisema Ritha Kabati.

Kutokana na kutajwa kwa majina hayo, Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliomba kumpa taarifa mbunge huyo. Alisema Kambi hiyo inapoibua jambo haijalishi litamgusa kiongozi wa chama gani ili mradi tu liwe na manufaa kwa taifa.

“Kambi ya upinzani inapoibua jambo huwa linakuwa kwa maslahi ya Taifa. Hivyo, ni vema wabunge wote mtambue kuwa kosa likifanywa na kiongozi buila kujali ametoka Chadema, CUF au CCM… tunapotoa uamuzi kama kambi ina maana sheria ifuate mkono wake,” alisema Mbowe.

Awali, katika hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia, alitaka serikali ichukue hatua stahiki kwani licha ya kuuza nyumba 7,921 wakati huo, iliweza kujenga nyumba 650 tu.

Kauli ya Mbatia iliungwa mkono na mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM) aliyehoji utaratibu uliotumika kuuzwa nyumba hizo huku akiitaka Serikali kufanya uamuzi wa kuzirejesha ili wapewe watumishi.

Mbunge CCM anusurika kupigwa na Wabunge wa Viti Maalum Ukawa
Uteja wa Simu wamponza bibi harusi, atalakishwa saa chache baada ya ndoa kwa kuchat usiku mzima