Hatimaye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amekutana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuzungumza naye kuhusu mazungumzo yake na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Lowassa imewataka wananchi kupuuza uzushi unaoenea mitandaoni kuhusu mwanasiasa huyo.

“Taarifa zinazosemwa mitandaoni zikionesha kuwa zimetoka kwa msemaji wa Lowassa sio za kweli kutoka ofisini kwa Mh. Lowassa. Baada ya ziara ile, mheshimiwa Lowassa alikutana na mwenyekiti wa chama chake, Freeman Mbowe na kumpa mrejesho wa yaliyojiri ikulu,” imeeleza taarifa hiyo.

Ameongeza kuwa kumekuwa na hatua hata za kufungua akaunti feki kwenye mitandao ya kijamii hivyo taarifa hizo zipuuzwe kwani zimelenga katika kupotosha kwa malengo ambayo wapotoshaji wanayojua wenyewe.

Awali, Mbowe alieleza kutokubaliana na kile alichokisikia kikisemwa na Lowassa alipokuwa Ikulu akieleza kuwa sio msimamo wa chama bali ni mawazo yake binafsi. Pia, alikiri kuwa Lowassa hakutoa taarifa kwenye chama kuwa atazuru Ikulu.

Hata hivyo, alisema kuwa hatua alizochukuwa Lowassa hazikuwa na ulazima wa kuomba kibali kwenye chama na kwamba alichozungumza ingawa kinatofautiana na msimamo wa chama, ana haki ya kutoa maoni yake.

Akiwa Ikulu, Lowassa alisifu juhudi na kazi ya Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na anachokifanya kwenye sekta ya elimu na mpango wa kujenga reli ya kisasa kuwa italeta ajira nyingi kwa Watanzania.

Kanisa tajiri Botswana lafungiwa
Kibatala ajiengua uwakili kesi ya Wema Sepetu