Kocha Mkuu wa Young Africans Luc Eymael, ameendelea kusisitiza kuwa, mchezo wa kesho kwake ni muhimu zaidi kuliko michezo mingine waliyocheza msimu huu 2019/20.

Eymael amesema si kama wanahitaji kuendelea kuifunga Simba, lakini wanahitaji kusonga mbele katika michuano ya Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC), ili watimize malengo ya kuchukua ubingwa na kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kocha Eymael ameyasema hayo baada ya kuwasili Dar es salaam na kikosi chake akitokea mjini Bukoba-Kagera alipokua ameweka kambi ya siku mbili baada ya kukamilisha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguuko wa 34 dhidi ya Kageraa Sugar, waliokubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

“Ni mechi muhimu sana kwa Yanga, ni mechi ambayo itatupa mwelekeo wa kushiriki mashindano ya kimataifa, tunahitaji kushiriki mashindano ya CAF msimu ujao, hii ndio nafasi pekee tuliyonayo ili kufikia malengo, hatutaki kumaliza msimu huu bila kikombe, baada ya kupoteza taji la Ligi Kuu,” Eymael alisema.

Mbelgiji huyo amewataka mashabiki wa Young Africans kutokuwa na hofu na kuendelea kuungana ili wapate ushindi.

Mchezo huo utakuwa watatu kuwakutanisha msimu huu baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka sare ya mabao mawili kwa mawili, na waliporudiana Machi 8, mwaka huu, Young Africans walipata ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Mchezo wa kesho ni mchezo wa mashindano yanayochezwa kwa mfumo wa mtoano na bingwa wake hupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Licha ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa haijamalizika, mabingwa wa msimu huu, Simba watashuka dimbani tayari wakiwa na tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo yanasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Mchezo mwingine wa hatua ya Nusu Fainali ya michuano hiyo utachezwa, leo Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga kati ya wenyeji Sahare All Stars dhidi ya Namungo FC kutoka Lindi.

Fainali za michuano hiyo zitafanyika Agosti 02, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela ulioko Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Klopp: Jordan Henderson hadi 2020/21
Wakamilisha ndoa kwa njia ya mtandao, waifunga kipekee