Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wanaosambaza taarifa za uongo kuhusu kutekwa au kupotea.

Akizungumza jana mjini Bunda mkoani Mara, Lugola ambaye alikuwa anajibu swali la mwananchi aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kukomesha matukio ya watu kutekwa au kupotea, alisema taarifa za matukio hayo nyingine hutungwa na watu kwa ajili ya kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Alisema kuwa taarifa za matukio hayo zipo za aina mbili na kwamba aina mojawapo ni ya uongo unaotengenezwa na baadhi ya watu kwa lengo la kujipatia umaarufu. Alieleza kuwa jeshi la polisi limewafikisha mahakamani baadhi ya watuhumiwa.

“Miongoni mwa wanaodaiwa kutekwa au kupotea wengine tumewabaini wanajiteka wenyewe,” alisema Lugola.

“Wapo waliofikishwa mahakamani kwa kutoa taarifa za uongo kuwa wametekwa au kupotea,” aliongeza.

Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na taarifa za watu kudaiwa kutekwa na baadaye kupatikana akiwemo Raphael Ongagi ambaye ni msaidizi wa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Allan Kiluvya ambaye ni msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bernard Membe.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kuwa taarifa za kutekwa kwa wasaidizi hao zinatia shaka kwa jinsi walivyotoa maelezo baada ya kudai wameachiwa na watekaji. Hata hivyo, alisema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kubaini ukweli.

Aidha, wapo baadhi ya watu walioripotiwa kupotea na hawajapatikana. Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema na mwandishi wa gazeti la The Citizen/Mwananchi, Azory Gwanda ni miongoni mwao.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi.

AFCON: Fainali ni Algeria na Senegal
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 15, 2019