Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya wizara yake kuwaondoa mara moja wananchi wote waliovamia katika maeneo ya majeshi nchini.

Ameyasema hayo mara baada ya kukagua Gereza jipya la Wilaya ya Ruangwa linalojengwa ambalo lina ekari 100 lakini ekari 20 zimevamiwa kwa kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya Alizeti, Ufuta na Korosho katika eneo hilo la Jeshi la Magereza.

Akizungumza baada ya kulikagua Gereza hilo mjini Ruangwa, Lugola amesema kuwa kuanzia sasa viongozi wa vyombo vyake wahakikishe hawaruhusu mwananchi yeyote kuingia katika maeneo ya jeshi na atakua mkali kulifuatilia suala hilo.

“Mimi huwa nashangaa sana inakuaje wananchi wanavamia ardhi ya jeshi tena bila woga, halafu jeshi linakaa kimya linabaki kunung’unika, hii haijakaa sawa kabisa na kamwe sikubaliani nalo,” amesema Lugola.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza mkoani humo, Rajabu Nyange amesema kuwa licha ya ujenzi wa gereza hilo kuendelea kujengwa lakini ekari 20 ilichukuliwa kimakosa na kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti na ufuta pamoja na kubangua korosho vinavyomilikiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

 

Video: Dar Chungu kwa Makonda, Jaji kesi ya bilionea Msuya atishiwa kuuawa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 27, 2018