Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola jana alitoa mtazamo ambao unakinzana na ule wa Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako kuhusu mafahari wawili wa Bongo Fleva, Diamond na Ali Kiba.

Jana, Waziri Lugola alizua gumzo baada ya kueleza kuwa kwa sasa hawezi kutaja nani zaidi kati ya wawili hao lakini anaweza kutumia kigezo cha nidhamu kuwatofautisha.

Alisema kwa mtazamo wake, Diamond hana nidhamu ya kazi ukimuweka na Ali Kiba kwenye mzani wa kigezo hicho.

“Ali Kiba na Diamond… mimi niwashindanishe kinidhamu. Ali Kiba ana discipline(nidhamu); na Diamond aliwahi kulalamikiwa na wenzetu kwamba amekuwa akichelewa kwenye jukwaa,” Waziri Lugola ameiambia Mwananchi Digital.

Aliongeza kuwa kutokuwa na nidhamu kunaweza kuathiri kazi ya msanii hata kama anafanya muziki mzuri unaoweza kuwainua mashabiki kwenye viti.

Mtazamo huo wa Waziri Lugola umekuja takribani miezi miwili baada ya Mzee wa Upako kuzua gumzo aliposema kuwa Ali Kiba ana kiburi tofauti na alivyo Diamond kuwa ni mnyenyekevu.

“Mimi nampenda sana Diamond kwa sababu ni mnyenyekevu, simpendi Alikiba sababu ana kiburi, nadhani kwa sababu amekaa kariakoo. Ukimpiga simu Diamond anapokea kwa unyenyekevu ila Alikiba anapokea kwa maringo. Ndo maana Diamond amefika mbali,” Mchungaji Lusekelo aliiambia Times FM.

Kauli ya Mzee wa Upako ilimuibua Ali Kiba ambaye alisema kuwa yeye anaishi atakavyo na uhalisia wa alivyo na hataki mtu ampangie namna ya kuishi kwani wakati anahangaika kuyafukuzia mafanikio hakusaidiwa na watu hao.

Kukinzana kwa mitazamo kati ya Mzee wa Upako na Ali Kiba kunaonesha namna ambavyo watu huweza kumchukulia msanii kwa mtazamo tofauti na huenda ndio sababu hasa inayowafanya wafuasi wao kutofautiana hasa unapotoka wimbo wa mmoja kati ya wasanii hao wanaochuana vikali.

Kisa cha mwanamke aliyekataa kuolewa na mwanaume aliyemtolea figo
Luis Nani arudi nyumbani